Maagizo aliyoyatoa Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Kassim alipokuwa ziarani Mkoani Iringa katika Kijiji cha Idodi Halmashauri ya Wilaya ya Iringa yametekelezwa.
Wataalamu kutoka Idara ya Ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Iringa wakiongozwa na Mkuu wa Idara hiyo Bw. Evidence Machenje walifika katika Kijiji cha Kitisi (Idodi) siku ya Jumatatu tarehe 30.09.2019 na kufanya mkutano na Wajumbe wa Halmashauri za Vijiji viwili vyenye Mgogoro wa kimpaka ambavyo ni Kitisi na Mapogoro ili kufikia muafaka wa mgogoro huo wa muda mrefu wa kugombea mpaka.
Wajumbe wa Vijiji vyote viwili walikubaliana kukaa kikao cha pamoja siku ya Jumatatu tarehe 07.10.2019 ili kupitia upya mpaka kati ya Vijiji vyao ambao unaleta mgogoro, na makubaliano watakayokuwa wamefikia katika kikao hiko yapelekwe kwa Mkuu wa Idara ya Ardhi wa Halmashauri ili arudi tena Kijijini hapo kuweka rasmi mpaka watakaokuwa wameridhia Vijiji vyote viwili, ambapo Mkuu wa Idara ya Ardhi ameomba kabla ya tarehe 15.10.2019 awe amepata makubaliano yao kwa ajili ya kuumaliza mgogoro huo na kupeleka taarifa kwa Mhe. Waziri Mkuu.
Aidha Maafisa wa Polisi walifika katika Kijiji cha Idodi Siku ya Jumatatu tarehe 30.09.2019 na kuwakamata Viongozi wa Jumuiya ya Watumia maji ya Matunguru ambao wanatuhumiwa kufanya ubadhirifu wa shilingi milioni 7.
Katika Ziara yake Mkoani Iringa tarehe 28.09.2019 Mhe. Waziri Mkuu alliongea na Wananchi wa Kijiji cha Idodi katika Mkutano wa hadhara, ambapo katika Mkutano huo ziliibuka tuhuma dhidi ya Viongozi wa Jumuiya ya Watumia maji kutafuna shilingi milioni 7, hali iliyopelekea Mhe. Waziri Mkuu kutoa maagizo ya kukamatwa kwa Viongozi wote wa Jumuiya hiyo waliojihusisha na ubadhirifu huo.
Pia liliibuka sakata la mgogoro wa kimipaka wa muda mrefu kati ya Vijiji vya Kitisi na Mapogoro, ambapo Mhe. Waziri Mkuu alimwagiza Mkuu wa Idara ya Ardhi wa Halmashauri kufika mara moja Kijijini hapo na kutatua mgogoro huo.
Mtaa wa Gangilonga
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0754 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa