DED Iringa ateta na Watendaji, Waratibu na Wakuu wa Shule
Ummi Mohamed na Antoni Ramadhani (Ofisi ya Habari na Uhusiano-Iringa DC)
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Wakili Bashir Muhoja Oktoba 6 mwaka huu amekutana na Watendaji wa Kata,Waratibu wa elimu na Wakuu wa shule kwa lengo la kupitia na kuweka maandaliza mazuri kwa ajili ya miradi na kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2022.
Akizungumza katika kikao kazi hiko Wakili Muhoja amesema pamoja na kutambua kazi nzuri wanazofanya lakini wanatakiwa kujiwekea mipango mizuri itakayopelekea kutokuwepo na changamoto ya upungufu wa madawati katika shule zao.
“Namshukuru sana Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Samia Suluhu Hassan kwa kuona changamoto ya madarasa katika maeneo mengi na sisi Halmashauri ya Wilaya ya Iringa tupo katika neema ya madarasa hayo tuna mshukuru sana”alisema na kuongeza;
Kuhusu maandalizi ya Miradi Mkurugenzi amesema kuwa anatarajia kuanza kutembelea shule zote hivi karibuni na amewataka watendaji na waalimu kujiandaa na kuwaandaa watoto. Aidha ameongezea kwa kutoa rai juu ya matumizi sahihi ya fedha.
“Wengine wanajiuliza kwa nini tunazungumzia fedha ambazo hata bado hazijafika, ni vizuri kuanza maandalizi mapema kwa sababu hatuna muda, lakini pia ni lazima kuzingatia matumizi sahihi ya fedha”
Amewataka pia Waalimu wakafanye maandalizi mazuri kwa wanafunzi ili waweza kufanya vyema mitihani yao kwa kutumia yale waliofundishwa kwa kipindi cha miaka mine kwa kidato cha nne. na miaka miwili kwa kidato cha pili na sio kuwafundisha ama kuwaandaa kufanya mitihani hiyo kwa udanganyifu.
Nae Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya Mwl.Hamis Mapoto amesema katika mtihani wa utamilifu matokeo hayakuwa mazuri hususani kidato cha pili kwa kuwa na ufaulu wa 58% na GPA 4.08 huku kidato cha nne wakiwa na ufaulu wa asilimia 92.9 na GPA ya 3.55.
“Matarajio yetu ilikuwa ni watoto wafaulu zaidi ya hayo matokeo, walimu tusibweteke tuwe karibu na watoto wetu na kuwapatia msaada wa kila hali ili wafaulu vyema kama ambavyo tumetarajia na kuwawezesha kufanya mitihani kwa kijiamini na sio kuibia.” alisema.
Aidha Mwl.Mapoto aliwapongeza na kuwataka wafanye kazi zote kwa kushirikiana ili kubaini kama kuna changamoto zinazowakabili wanafunzi na kuzipatia ufumbuzi mapema kabla hazijaathiri maandalizi ya wanafunzi au mwananfunzi husika.
Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kama Halmashauri zingine zinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo uhaba wa madawati na vyumba vya madarasa.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa