Care International Yawaondoa Wananchi Kwenye Kilimo cha Mazoea
Care International ni Shirika Binafsi linalofanya kazi kwa kushirikiana na Serikali katika kuwahudumia wananchi kwa mahitaji mbalimbali. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Care International inafanya kazi katika Vijiji 62 kwa shughuli mbalimbali zikiwemo za kilimo.
Care International imeanzisha mashamba darasa katika vijiji 18 kwa kuwawezesha Wagani Kazi kupitia mradi wa FFBS, kwa kulima cha mazao ya soya na alizeti.
Lengo la mradi ni kuwafundisha wananchi kuondokana na kilimo cha mazoea, na kufanya kilimo cha kisasa ambacho kitaweza kuwapatia kipato kupitia zana za; Kilimo bora, Jinsisa, Lishe, Biashara na Masoko.
Baadhi ya Vjiji vilivyokuwa na Mashamba Darasani ni Ikuvilo Kata ya Luhota, ambapo kuna kikundi cha Jiongoze. Kijiji cha Ng’enza Kata ya Magulilwa kuna Vikundi vya Faraja, Kikundi cha Ushirikiano na Kikundi cha Urafiki. Kijiji cha Lyamgungwe Kata ya Lyamgungwe kuna Kikundi cha Umoja ni Nguvu na Kikundi cha Songambele. Kijiji cha Makota Kata ya Masaka kuna kikundi pia na Waganikazi, Pia katika Kijiji cha Mangawe Kata ya Nyang’oro kuna Kijiji cha Umoja.
Akitoa salamu za pongezi Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Stephen Mhapa amesema, “Nawapongeza Care International kwa kufanya kazi katika Halmashauri yetu. Kati ya Vijiji 134 ni vijiji 62 vinafaidika na shughuli za Care. Nawaomba Care International kuwafikia vijiji vyote 134 ili Halmashauri nzima iwe imafaidika na huduma hizi”.
Mheshimiwa Mhapa amewashukuru Madiwani wa Kata zote ambazo kuna miradi hii ya Care International na kuwasisitiza wananchi kufanya kilimo cha kitaalamu zaidi ili kupata mazao mengi.
“Mnavyolima tumieni utaalam huu ambao mmejifunza kwa kutumia ardhi kidogo na kupata mazao mengi. Viongozi wote ngazi zote wawe mfano ili wananchi waweze kujifunza kutoka kwenu”.
Akizungumzia mradi huo, Mratibu wa Mradi Ndugu Peter Pasifiki amesema, “kupitia mradi huu tunategemea kuona jamii inabadilika katika suala zima la kilimo. Mradi utadumu kwa muda wa miaka mitatu hivyo kufanya jamii ichukue mbinu za uzalishaji ili kuwe na maendeleo endelevu. Tija ya mradi huu itasaidia jamii kuwekeza na kupiga hatua”.
Ndugu Pasifiki ameendelea kusema kuwa, “soya na alezeti itasaidia kuwanua watu kipato chao, pia kutokomeza udumavu katika jamii. Akina mama wapewe nafasi ya kutosha katika kukuza jamii, na wanaume wana nafasi ya kubadilisha jamii kupitia mradi huu”.
Naye Afisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Bi. Lucy Nyallu amesema, “tuachane na kilimo cha mazoea na tufuate kilimo chenye tija.Kupitia mradi huu tutapata kipato na kukuza familia. Pia kuweka lengo katika msimu ujao”.
Bi. Lucy ameendelea kusema, “Agenda 20/30, Kilimo ni Biashara, ambapo ndiyo Kauli Mbiu ya Kilimo. Care International wanashirikiana na Serikali katika jambo hili, hivyo tunasimama nao pamoja ili kutoa elimu juu ya kilimo bora chenye tija”.
Aidha Diwani wa Kata ya Masaka ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Meshimiwa Methew Nganyagwa ametoa neno kuwa, “Baada ya shule ni mtahani, hivyo mwakani muda kama huu tutakuja kukagua tuone mtihani huu kama mmefaulu”.
Mheshimiwa Nganyagwa ameendelea kwa kutoa ombi la matengenezo ya barabara inayotoka Tanangozi hadi Makota yenye urefu wa Kilometa 20 na kutoka Makota hadi Ihemi yenye urefu wa kilometa 7.
Pia Waheshimiwa Bruno Kindole wa Kata ya Luhota, Mheshimiwa Alex Malangalila wa Kata ya Lyamgungwe, Mheshimiwa Jane Mhangala wa Kata ya Magulilwa, Mheshimwa na Mheshimiwa Elizabeth Ngole wa Kata ya Nyang’oro wakiwa na Washimiwa Madiwani wa Viti Maalum, Mheshimiwa Anitha Magelanga, Mheshimiwa Yuster Kinyaga na Mheshimiwa wameishukuru Serikali kwa kuwaruhusu Care International kutoa nafasi kufanya kazi kwa wananchi na kuwapatia fursa hii ambayo wataitumia vizuri. Kilimo hiki kitasaidi kuondoa udumuvu na kuwaingizia kipato.
Akitoa ombi kwa niaba ya wananchi Victory Alberto amesema, wanaomba kutengenezewa mfereji wa Mkombozi ambao utatusaidia kufanya kilimo cha umwagiliaji wakati wa kiangazi na kufanya misimu miwili ya kilimo, na kwamba wakifanya hivyo wataweza kubadilika kiuchumi kwa haraka zaidi.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa