DAS Estomin Afurahishwa, IDC Hakuna Kaya Isiyo na Choo
Katibu Tawala Wilaya ya Iringa Ndugu Estomin Kyando amepongeza juhudi za Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwa kufanikiwa katika kusimamia na kuhakikisha kila kaya ina choo. Amesema kuwa ni aibu kusikia kuwa kaya kadhaa hazina vyoo lakini kwa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imekua ni tofauti kwani Kaya zote zina vyoo.
Ameyasema hayo katika ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya usafi na siku ya matumizi ya choo duniani ambayo huwa yanaadhimishwa kila tarehe 19/11. ambapo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa yameadhimishwa tarehe 12/11/2022 katika Kata ya Kalenga Kijiji cha kalenga na kuendelea mpaka siku hiyo ya kilele.
Ndugu Estomin amesema kuwa Magonjwa mengi yanatokana na uchafu wa mazingira ikiwemo kipindupindu, kuhara nakadharika hivyo tukiwa na vyoo bora na matumizi sahihi tutaepukana na magonjwa hayo kadhalika tutalinda afya zetu, na pia tutakua tumepunguza gharama za matibabu kwa sababu ukiugua lazima utibiwe.
"Tunafanya haya maadhimisho tukiwa katika hali nzuri, tuko kwenye asilimia 89.3, tuna kila sababu ya kuwapongeza wananchi na Mkurugenzi nae na timu yake ya wataalamu tunakupongeza sana Hongereni sana"
Lakini pia ametoa wito kwa wananchi ambao wana vyoo lakini si bora amewataka kuboresha vyoo vyao. Aidha amewaagiza wataalamu kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuwa na vyoo bora, choo bora ni cha namna gani na athari zinazoweza kutokea kutokana na kutokua na vyoo bora ili waweze kuboresh vyoo vyao na tufike asilimia 100.
Akisoma taarifa ya uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya usafi na siku ya matumizi ya choo duniani Bibi Gladness Amulike amesema Katika masuala ya usafi wa mazingira Halmashauri yetu imekuwa ya kwanza kuwa na vijiji vingi vilivyofikia madaraja ya ubora ya usafi wa mazingira(ODF) kitaifa, vijiji 75 kati ya 134 ndio vimeweza kupata vyeti mpaka sasa.
"Halmshauri yetu ipo kwenye mpango wa kufikia asilimia 100 ya kaya zote kujenga vyoo bora na kutumia, na kuwa na vifaa vya kunawa mikono vya maji tiririka na sabuni. Pia vijiji vyote kuweza kupata madaraja ya ubora wa usafi wa mazingira(ODF) ifikapo Disemba 2022."
Nae Diwani wa Kata ya Kalenga Mhe. Shakira Kiwanga amesema Kijiji cha Kalenga na Kata kiujumla bado wanendelea na uhamasishaji wa matumizi ya choo bora na kuwataka wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo kuwa mabalozi wazuri kwa ambao hawajadhuria wakawapatie ujumbe mzuri uliowasilishwa kuhusu matumizi ya choo bora.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Wakili Bashir Muhoja amewashukuru wananchi wa Kalenga kwa michango yao ambayo wameendelea kuchanga kwa ajili ya maendeleo ya Kata, Ujenzi na ukarabati wa madarasa pamoja na kituo cha afya amesema kwa sasa mambo ni safi.
Aidha ametumia uwanja huo kutoa wito kwa wazazi na wananchi wa kalenga kuwaombea Wanafunzi wa kidato cha nne wanaokwenda kuanza mitihani yao ya kuhitimu elimu ya sekondari kuanzia tarehe 14.11.2022.
"...Lakini pia mtakumbuka hapa tunayo Sekondari ya Lipuli na jumatatu watoto wetu wanakwenda kuanza mitihani yao, ninawaombeni sana tuwaombee watoto wawe na utulivu wafanye mitihani yao ili watengeneze maisha yao ya kesho”.
kwani wakifaulu kweti sisi ni neema, Hivi viti tulivyovikalia sasa hivi tunaelekea kuviacha kwa kadri siku zinavokwenda hivyo yatupasa kuwaandaa warithi wetu na kuwaandaa ni pamoja na kuwasomesha". Amesema Mkurugenzi Mtendaji.
Maadhimisho ya wiki hii ya usafi na siku ya matumizi ya choo yenye kauli mbiu ya “Kufanya yasiyoonekana kuonekana”. yameadhimishwa huku zoezi la usafi wa mazingira la pamoja limefanyika katika maeneo yote ya Halmashauri, ikiwa na lengo la kuadhimisha wiki hii kwa vitendo na kuweka mazingira safi.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa