DC Kheri, Afanya Ziara Tarafa za Kiponzero, Kalenga na Mlolo, Asisitiza Mambo Matano
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Kheri James, ameendelea kufanya ziara katika Tarafa za Halmashauri ya Wilaya ya Iringa na kuongea na wananchi na Watumishi mbalimbali
Lengo la ziara hiyo ni kujitambulisha kama Mkuu wa Wilaya Mpya na kujionea maeneo ya utawala wake, baada ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya mabadiliko katika nyanja mbalimbali za uongozi.
Katika ziara yake Mheshimiwa Kheri amesisitiza mambo matano muhimu ambayo Watumishi wanatakiwa kuyafuata katika utendaji wao wa kazi. Amesema, “Jambo la kwanza katika utendaji wa kazi ni Utawala wa Sheria, kila Mtumishi afanye kazi kwa kufuata sheria, taratibu na miongozo tuliyojiwekea ili kuepukana na usumbufu wa hapa na pale. Mtumishi anatakiwa kufuata misingi iliyopo na kuwepo mahala pa kazi muda wote ambao anatakiwa kuwepo. Pili Haki, kila mtu atapata haki kulingana na jambo husika, hakuna mtu kuonewa au kumuonea mwingine kwa sababu hakuna mtu aliye juu ya sheria. Tatu Usawa, hii itasaidia mtu kufanya kazi kwa uadilifu bila kubaguana kabila, dini, rangi wala jinsi. Nne Maendeleo, katika kujiletea maendeleao tunatakiwa kufanya kazi kwa kushirikishana na bila kutegea na jambo la Tano Umoja na Mshikamano, katika kazi zetu tunatakiwa kushirikiana na kushikamana ili kuleta maendelea na hatimaye kufikia malengo tuliyojiwekea, amesema Mheshimiwa Kheri.
Mhe. Kheri hakuacha kusisitiza suala la lishe, amewataka wananchi kula chakula chenye mlo kamili ili kujiletea afya njema. Amesema, mtu asipokula vizuri na kukosa lishe anakosa uwezo wa kufikiri hata kushindwa kufanya kazi. Hivyo amesisitiza hasa kwa watoto wapate chakula chenye mlo kamili.
Aidha, Mheshimiwa Kheri amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Watumishi waliopo katika maeneo yao, ili wafanye kazi kwa moyo mmoja na kuwahudumia kwa upendo. Amewataka wananchi hao kutoa ushirikiano ili kama itatokea sintofahamu basi jambo hilo liweze kutatuliwa kwa pamoja.
Kadhalika Mheshimiwa Kheri aliweza kutoa nafasi kwa wananchi kuuliza maswali na kutoa kero zao, ambapo kero mbalimbali na migogoro ilitolewa na Mheshimiwa aliweza kuchukua hatua stahiki.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa