DC Moyo Aagiza Watoto Kupatiwa Chakula Mashuleni
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Mohammed Moyo ametoa maagizo hayo katika kikao cha tathmini ya mkataba wa lishe kwa robo ya kwanza (Julai - Septemba 2022) kilichofanyika terehe 21.10.2022 katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Iringa.
Amesisitiza na kutoa maagizo kwa watendaji walipokuwa wakisaini mkataba wa lishe na Mkurugenzi Mtendaji kuhakikisha kuwa mkataba wa lishe uendane na hali halisi kwa kuhakikisha kuwa kila shule inatoa chakula kwa wanafunzi ili kujiepusha na madhara yatokanayo na ukosefu wa lishe kama vile udumavu na utapia mlo.
"Nendeni mkazingatie sheria, msicheke na wazazi, watoto lazima wapate chakula wakiwa shuleni na wazazi lazima wachangie kwa kuzingatia sheria, nyinyi kazi yenu ni kwenda kusimamia sheria hiyo ili watoto hawa wajiepushe na athari zitokanazo na ukosefu wa lishe".
Amesema kuwa kitaifa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imefanya vizuri sana, na hiyo yote ni kutokana na jitihada kubwa na juhudi zilizofanywa kufanikisha hilo hivyo amewataka Watendaji na Wataalamu kuendeleza jitihada na juhudi hizo ili kuweza kupanda zaidi.
Aidha amepongeza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa chini ya Mwenyekiti Mhe. Mhapa na Mkurugenzi Mtendaji Wakili Muhoja kwa kuhakikisha kuwa fedha iliyotengwa kwa ajili ya masuala ya lishe inawasilishwa kwa wakati na inatumika ipaswavyo.
"Ninajuwa mna mambo mengi lakini pia hamkuweza kulisahau hili la lishe hivyo ninawapapongeza sana na muendelee kufanya hivyo".
Lakini pia Mkuu wa Wilaya Mhe. Moyo amesisitiza Wataalamu kuendelea kutoa elimu na hamasa kwa wananchi kujisajili kwa ajili ya kupata mbolea ya ruzuku.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Wakili Bashir Muhoja amesema kuwa kuwajali watoto ni jukumu la wote na kama tusipowajali kwa kuwapatia lishe bora basi tutakuwa na kizazi cha hovyo kwa hapo baadae.
" Hawa watoto kwa hapo baadae watakuja kuwa kwenye meza ya maamuzi hivyo tuwaandae hawa watoto na kuwaandaa ni pamoja na kuwafanya wawe na bongo nzuri na bongo nzuri inatokana na lishe".
Naye Afisa Lishe Wilaya Bibi Tiliza Mbula ameshukuru Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kuweza kusimamia vyema na kuifanya Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kufanya vizuri kitaifa kadhalika amewaomba na kuwataka watendaji kuendelea kuhamasisha lishe kwa wanafunzi ili Halmashauri iweze kufanya vizuri na ipande nafasi za juu zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji Wakili Muhoja amesaini na kukabidhi mikataba ya lishe kwa Watendaji wa Kata za Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwa lengo la kufanya utekelezaji kwa robo ya pili ya mwaka wa fedha 2022/2023.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa