Eng. Mativila Atembelea Iringa DC
“Nimefurahi kufika kujionea jengo hili jipya ambapo nimeweza kujionea mazingira na miundombinu yote. Pamoja na mambo mengine nimechukua changamoto zote mlizozitaja na nitaenda kuzifanyia kazi. Nawaomba muwe wavumilivu na muendelee kuchapa kazi kwani mnapopata kitu kipya changamoto huwa hazikosekani”.
Kauli hii imetolewa na Naibu Katibu Mkuu – Miundombinu kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Rogatus H. Mativila leo Novemba 13, 2023 alipotembelea Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kujionea miundombinu ya jengo la Makao Makuu ya Halmashauri hiyo lililopo Kijiji cha Ihemi Kata ya Mgama.
Akiwasilisha taarifa ya mradi huo wa jengo la Makao Makuu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Wakili Bashir Paul Muhoja amesema, “kwanza namshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kiasi cha Bilioni 3 ambazo zilitolewa kwa awamu na kuweza kukamilisha ujenzi, hatimaye Julai 31, 2023 huduma zilianza kutolewa rasmi katika jengo hilo jipya la Makao Makuu”. Pamoja na kuanza kutoa huduma, bado kuna kazi ndogondogo zinaendelea kama ujenzi wa ukuta”.
Wakili Muhoja ameendelea kusema kuwa, “pamoja na mafanikio ya ujenzi wa jengo hili, kumekuwapo na changamoto kadhaa zilizojitokeza ikiwemo maji, makazi ya watumishi, miundombinu ya barabara na uhaba wa vyumba, lakini tunaendelea kukabiliana nazo huku tukiendelea na mchakato kutafuta ufumbuzi wa kudumu”.
Mhandisi Mativila amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji kuandika barua ambayo itaainisha changamoto zote, kwenda kwa Katibu Mkuu TAMISEMI wakazifanyie kazi ili watumishi wafanye kazi bila kikwazo.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa