INADEC Yamuokoa Mnyama Punda Katika Asili Yake
INADEC ni Shirika la Kifaransa linalojihusisha na kustawisha maisha ya Mnyamakazi Punda, na ufugaji kwa ujumla. Shirika hilo limeandaa Jukwaa kwa Wafugaji na Wakulima kupitia vikundi mbalimbali.
Lengo kubwa la Shirikia hili ni kufikisha ujumbe na kutoa elimu kwa jamii, kwa kutumia vikundi hivyo, kwa kufanya mikutano, nyimbo, mashairi na shughuli mbalimbali za kijamii.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Shirika la INADEC limeweza kufanya kazi katika Kata mbili za Migoli na Izazi ambapo kuna wafugaji wakubwa wa Mnyama Punda. Kwa kuandaa Jukwaa hili, jamii imeweza kupata elimu juu ya malezi ya Mnyama Punda, kwani ni mnyama anayefanya kazi nyingi na kumuingizia kipato mwanajamii anayefuga.
Akifafanua haki za Mnyamakazi Punda, Afisa Mradi wa shirika la INADEC Ndugu Michael Kihwele amesema, “kuna mambo mengi ambayo yanaweza kumuathiri Mnyamakazi Punda. Pamoja na mambo mengine anahitaji kupatiwa haki zake mbalimbali zikiwemo, Kutobughudhiwa, kupewa chakula cha kutosha na maji mengi, kuishi kwa tabia zake za asili, kutoogopeshwa na kutopatiwa majeraha, maumivu na kupatiwa matibabu”.
Ndugu Kihwele ameendelea kusema kuwa, mnyama Punda anatakiwa kutunzwa vizuri kwa kumjengea banda ili aweze kupumzika mahala salama baada ya kazi, na kwamba banda liendane na mazingira halisi ili aweze kuwa faida kwa jamii. Pia kutokana na hali ya tabianchi, mfugaji analazimika kuandaa malisho kwa kulima nyasi kwa ajili ya chakula chake.
Naye Mratibu wa Mradi Ndugu Isdori Karia amesema, “mradi ulipoanza kulikuwa na changamoto ya wizi wa mnyama punda, kwani jamii aliamini punda anaweza kuliwa kama nyama nyingine hivyo kupelekea kuuzwa kwenye maeneo mbalimbali”.
Ndugu Karia ameendelea kusema kuwa, “kupitia jukwaa hili tuliweza kutoa uhamasishaji kwa vijiji vya Migoli, Makatapola, Izazi, Mangawe na Nyang’oro, na wananchi wameelewa umuhimu wa kufuga Mnyama Punda kwa kuwaeleza faida mbalimbali zinazopatikana kutokana na Punda”.
Ndugu Karia pia ameweza kufafanua kuhusu utunzaji wa punda ikiwa ni pamoja na kumuwekea ulinzi na kutomuumiza. Pia kuna Kliniki zimeanzishwa kwa ajili ya matibabu ya mnyama punda ili inapotokea ameumia au kuugua basi ni vizuri akapatiwa matibabu. Wataalamu 40 wa Ugani wamepatiwa mafunzo ya jinsi ya kumtibu mnyama punda. Wataalamu hawa wataweza kupita vijiji 134 vya Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya malezi ya Mnyama Punda.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wafugaji Mnyama Punda Bi. Spelancia Kinyaga naye alikuwa na haya ya kusema, “Mnyamapunda alikuwa hana uangalizi wa kutosha wa maisha yake na kazi. Kupitia INADEC tumeweza kujifunza jinsi ya kumuwekea mazingira mazuri na jinsi ya kumtuma kazi. Pia tumejifunza jinsi ya kumtumia punda kwa kutumia mkokoteni mwepesi, kwani mikokoteni inayotumika sasa ni mizito sana”.
Bi. Spelancia ameendelea kusema kuwa, changamoto ilikuwa ni wizi wa punda na kuchunwa ngozi yake kwenda kufanya biashara, kumpiga sana hadi kumsababishia majeraha”.
Manufaa yameonekana kupitia mnyama punda kwa kupata ruzuku mbalimbali kwa vikundi ambavyo vinaweza kufuga punda. Vikundi sita vilivyosajiliwa vimeweza kupata mikopo kutoka Halmashauri ya 10%, ili kuendeleza ufugaji wa Punda.
Pia kuna mashindano ya michezo mbalimbali imeanzishwa kwa ajili ya kufanya kampeni ya kumtangaza Mnyama Punda, ili jamii iwe na uelewa mpana juu umuhimu wake.
Jukwaa hilo limejiwekea mikakati mbalimbali ya ufugaji wa punda ikiwa ni kumuwekea mazingira mazuri, kumpatia haki zake, na vikundi kutekeleza mafunzo waliyofundishwa ya namna ya kumlea mnyama punda.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa