Jukwaa la Mafanikio Wilaya ya Iringa, Yaing’arisha Iringa
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Kheri James, amezindua Jukwaa la Mafanikio la Wilaya ya Iringa ambalo linahusisha Taasisi zote za Iringa kwa kutoa taarifa kwa wananchi wake ili wafahamu nini Serikali inafanya katika kuwaletea maendeleo.
Jukwaa hilo limezinduliwa Novemba 21, 2024 katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ambapo limekuwepo kwa muda wa siku sita mfululizo na pia litaendelea kila mwezi katika kutoa taarifa zake.
Akitoa hotuba yake katika Uzinduzi wa Jukwaa hilo Mhe. Kheri amesema, “Jukwaa hili ni kwa ajili ya kuhabarisha Umma, na kuondoa urasimu kwa wananchi, pia kutoa taarifa sahihi zinazofanywa na Taasisi ndani ya Wilaya. Wananchi wanapokuwa na taarifa sahihi wanafahamu vizuri juu ya nini Serikali inafanya, pia ni njia ya kuisogeza Serikali kwa wananchi”.
Mhe. Kheri ameendelea kusema, “Hapa tutafahamu kama kero za wananchi zinaifikia Serikali na zinatatuliwa kwa wakati kama barabara, Tanesco, maji nk. Kupitia Jukwaa hili tutaijenga Iringa kwa Umoja na Uwajibikaji, na kwamba kila mwisho wa mwezi Taasisi zote tutakutana hapa na kuweza kutoa taarifa zake, hivyo itasaidia kuwa Iringa ya mfano”.
Katika Jukwaa hilo wageni mbalimbali wamealikwa kwa makundi ili kuja kujionea Serikali ya Awamu ya Sita inatekeleza kwa kiasi gani katika kuwapatia wananchi wake maendeleo.
Taasisi zilizohusishwa katika Jukwaa hilo ni Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Wakala wa Barabaza Tanzania (TANROADS), Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA), Mamlaka ya Maji Mjini (IRUWASA), Mamlaka ya Maji Vijijini (RUWASA), Umwagiiaji, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Tanesco, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Taasisi hizo zote zimepata nafasi ya kutoa taarifa ya nini kinafanyika, ili kuwapa wananchi upeo wa kufahamu na haki ya kupata taarifa kwa kila Taasisi.
Wageni walihudhuria na kupata nafasi ya kutembelea miradi mbalimbali ambayo inatekelezwa na Serikali, pia walipata nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali na kutolewa ufafanuzi.
“Iringa Imara, Tutaijenga kwa Umoja na Uwajibikaji
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa