Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango Yatembelea Kata ya Migoli Kukagua Maendeleo ya Kata
Kamati hiyo imetembelea Kata ya Migoli tarehe 19/09/2022 kwa ajili ya kuongea na Wataalam wa Kata hiyo juu ya miradi ya Maendeleo.
Kati ya mambo ambayo yameongelewa katika kikao hicho ni pamoja kuwakumbusha kuwa, Wataalam na Diwani wa Kata hiyo Mheshimiwa Benitho Kayugwa kusimamia kwa umakini miradi ya maendeleo ili kufanikisha maendeleo ya wananchi.
Akiongea katika kikao hicho Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Steven Mhapa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo amesema, “Maendeleo ya Kata yanatokana na usimamizi mzuri wa ninyi Wataalam, hivyo mnapaswa kuwa mstari wa mbele katika usimamizi. Diwani na Wataalam lazima muwe na mawasiliano ya pamoja katika suala zima la utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hivyo siyo sawa kupishana kauli na kupelekea mgongano wa utekelezaji na kusababisha sintofahamu kwa wananchi”.
Mheshimiwa Mhapa ameongeza kusema kuwa, “heshima ni kitu cha msingi sana, yatupasa kuheshimiana bila kujali cheo wala nafasi uliyopo. Pia kuwe na mipaka katika masuala ya kazi. Kila mtu afanye kazi kulingana na mipaka yake ya kazi inapoishia”.
Aidha, Mheshimiwa Mhapa ameongelea suala la siasa akisema, “Madiwani ndiyo tunatakiwa kufanya siasa na si Wataalamu. Pamoja na kuwa viongozi wengi wanatokana na siasa, lakini Mtumishi wa Umma hatakiwi kuwa Mwanasiasa kwani yeye ni Mtendaji, na kufanya kazi kwa kadri taratibu zinavyomtaka na siyo kuleta siasa”.
Aidha Mheshimiwa Mhapa amewata watumishi wasiwe wanatoleana maneno makali na lugha zisizofaa, hata kama kuna jambo limekufanya uwe na hasira hadi kupelekea maumivi ya moyo, vumilia na kutafuta namna ya kulitolea ufumbuzi.
Kadhalika, Mheshimiwa Mhapa ametoa shukrani kwa wajumbe wa Kamati hii kwa kujitoa na kushiriki vema katika kuchangia hoja zilizopo katika kikao hicho.
Naye Diwani wa Kata hiyo Mheshimiwa Benitho Kayugwa amesema, “nipo tayari kwa kila jambo kushirikiana na Wataalamu ili kuendeleza gurudumu la maendeleo katika Kata yangu ya Migoli. Nitashirikiana vema na Mtendaji wa Kata hii na Watendaji wa Vijiji vyote vya Migolo”.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Bi. Beatrice Augustine alikuwa na haya ya kusema, “pamoja na mambo mengine yote, ni vizuri kila mtu asimame katika nafasi yake na ajue haki na wajibu wake. Tukitambua hili kila mtu atafanya kazi kwa raha na hakutakuwa na manung’uniko yoyote”
Bi. Beatrice amewasihi watumishi kufanya kazi kwa kupendana na kuchukuliana, kufanya kazi kwa bidi ili kuleta tija kwa maslahi mapana ya wananchi katika maendeleo.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa