Kamati ya Siasa Mkoa wa Iringa, Yapongeza Utekelezaji wa Miradi Inayoendelea Kutekelezwa Halmashauri ya wilaya ya Iringa
Kamati ya Siasa ya Mkoa imefanya ziara na kukagua miradi inayoendelea kutekelezwa katika Halmashauri. Kamati hiyo imefurahishwa na utekelezaji mzuri wa miradi hiyo, na kuona changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi.
Baadhi ya Miradi iliyotembelewa ni pamoja na mradi mkubwa wa ujenzi wa mfereji wa umwagiliaji katika Kata ya Itunundu na Mboliboli, Shule mpya ya Sekondari ya Mlenge inayojengwa kwa mradi wa SEQUIP, Hospitali ya Wilaya ya Iringa ambapo Kamati iliweza kufanya usafi kwa baadhi ya maeneo na jengo la Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ambalo limejengwa Kata ya Mgama.
Kamati hiyo imesifia miradi inayoendelea kutekelezwa katika Halmashauri, na kuwataka wananchi na watumishi waendelee kuunga mkono jitihada za Serikali kupitia Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajibika kila mtu katika eneo lake na kuondoa kero mbalimbali.
Akitoa Hotuba yake wakati wa majumuisho baada ya ziara Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wa Mkoa Mheshimiwa Daud Yassin Mlowe amesema, “ili Chama kifanye vizuri, kinategemea mahusiano mazuri na Watumishi wa Serikali, hivyo watumishi wasikwamishe huduma kwa wananchi na kupelekea kuichukia Serikali. Dosari ndogondogo zipo lakini zinarekebishika, hivyo sisi kama Serikali tusichochee wananchi kuichukia Serikali, kwani Serikali ina upendo mkubwa sana kwa wananchi wake na kupelekea kuletwa fedha nyingi kwa ajili ya miradi”.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mheshimiwa Halima Dendego amesema, “tunashukuru Kamati ya Siasa ya Mkoa kwa kufanya ziara na kutembelea miradi, kwani kufanya hivi kunatuongezea nguvu kubwa ya kufanya kazi. Sisi wajibu wetu ni kutenda kazi ya kuwahudumia wananchi, kwani sisi sote ni ndugu, pia kuendeleza agenda za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kama “Kumtua Mama Ndoo Kichwani, Kilimo, Elimu”.
Pia Mheshimiwa Dendego ametoa agizo kwa Mkurugenzi kuwa, wanafunzi wa Kidato cha Pili wa Shule ya Sekondari Pawaga ambao wanatokea Kata ya Mlenge wahamishiwe katika Shule mpya ya Sekondari Mlenge ili kuwapunguzia umbali wa kwenda na kurudi shule.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri Mheshimiwa Stephen Mhapa, amefurahi kuona viongozi wa Chama cha Mapinduzi kutembelea miradi na kujionea mafanikio na changamoto mbalimbali. Na kwamba Chama ndiyo Kiongozi hivyo tupo tayari kupokea maelekezo.
Mheshimiwa Mhapa pia amewapongeza watumishi kwa kufanya kazi vizuri wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Wakili Bashir Muhoja.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa