Kampeni ya Chanjo ya Polio Kitaifa Awamu ya Tatu (RD3), Yavuka Lengo la Mafanikio
Kamati ya Afya ya Msingi imekaa leo Oktoba 11, 2022 kufanya tathimini na kutoa taarifa ya Utekelezaji wa Kampeni ya Chanjo ya Polio Kitaifa Awamu ya Tatu (RD3), ambayo imefanyika mwezi Septemba. Kampeni hiyo ilijikita kupita nyumba kwa nyumba kwa ajili ya kuelimisha jamii na kutoa chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano juu ya ugonjwa wa polio.
Awamu ya Kwanza ya Kampeni hii ilifanyika kwa Mikoa inayopakana na nchi ya Malawi yaani Mbeya na Songwe, kwa sababu ugonjwa huu ulianza kulipuka nchini Malawi. Awamu ya Pili ya Kampeni imefanyika kwa Mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani ili kuwakinga watoto chini ya miaka mitano kutokana na ugonjwa huu ambapo lengo ni kuwafikia watoto zaidi 53,191 na kufanikiwa kuwachanja watoto zaidi ya 55,055 sawa na 103%.
Katika Awamu ya Tatu kwa malengo ya Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, iliazimia kuwakinga watoto zaidi ya 47,158 hivyo kuvuka lengo na kufanikiwa kuwafikia na kuchanja watoto zaidi ya 51,646 sawa na 110%.
Akitoa pongezi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Mohamed Moyo, ambaye ni Mwenyekiti katika Kamati hiyo amesema, “kwanza nawapongeza sana timu yote ya Afya kwa uhamasishaji na kutekeleza zoezi hili na kuvuka malengo tuliyojiwekea katika kuwachanja chanjo ya polio kwa watoto chini ya miaka mitano”. Pia amemuomba Mkurugenzi Mtendaji kuwapatia barua ya pongezi kwa Timu yote ya Afya kwa kufanya vizuri katika zoezi hili la chanjo.
Mheshimiwa Moyo ameongeza kusema kuwa, amealika na Kamati ya Ulinzi na Usalama ili waone umuhimu katika uhamasishaji wa zoezi hili pia wawe mabalozi wazuri kwa watu wengine.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Wakili Bashir Muhoja alikuwa na haya ya kusema, “pamoja na kuwa Halmashauri hii imetawanyika sana lakini Timu ya Afya ambayo inaongozwa na Mganga Mkuu, imepambana katika kuwafikia walengwa nyumba kwa nyumba, na hatimaye kuvuka lengo na kufikia 110%.” Hii inatia moyo sana na kuchukua suala la Mheshimiwa Moyo la kuwapatia barua za pongezi timu hiyo.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya Daktari Samwel Marwa amesema, “katika zoezi hili la utoaji wa chanjo safari hii tumefanya kitalaamu zaidi kuliko kipindi kingine chochote, kwani hakukuwa na ubabaishaji. Tumetumia vifaa ambavyo vimepima na kuonesha kuwa kila nyumba imechanja watu wangapi (GPS), hivyo hakuna upotoshaji wa taarifa”. Mganga Mkuu amemaliza kwa kuwashukuru Timu nzima ya afya na kuwaomba kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa