Nendeni Mkawajibike"- Muhoja
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Wakili Bashir Muhoja ameongoza kikao cha kujadili, kupokea maelekezo na ushauri juu ya mapokezi ya fedha kiasi cha Tsh 980,000,000/= kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya kidato cha kwanza 2023.
Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Halmshauri ya Wilaya ya Iringa (Siasa ni Kilimo) na kimekutanisha Wakuu wa Idara na Vitengo, Watendaji Kata, Maafisa Elimu Kata, Baadhi ya Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari pamoja na Maafisa Tarafa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.
Akifungua kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji Wakili Muhoja ambae pia amekuwa Mwenyekiti wa kikao amesema ameliita jeshi lake na anahitaji kuzungumza nao ili waweze kujipanga kwa lengo la kuaza kukimbizana na masuala ya ujenzi wa madarasa hayo.
Aidha amesema kuwa anataka kila mmoja afanye kazi kwa nafasi yake, kusiwepo na kutegeana kila mmoja akitimiza wajibu wake kutakuwepo na matokeo chanya.
"Ninawataka kila mmoja awe na taarifa kamili ya kile kinachoendelea katika ujenzi wa madarasa haya, Hamtakiwi kuwa nyuma ili hata unapoulizwa uwe na kitu cha kujibu".
Pia amewataka Watendaji kujitoa zaidi kufanya kazi kwa moyo na pale inapotokea kuna changamoto yoyote basi ni vyema kuwasiliana ili kuweza kutatua changamoto hiyo na sio kukaa nayo binafsi."
Tukisaidiana wote kazi hii itakuwa rahisi, Ninawaomba sana tujitoe ili tuweze kufikia malengo tumepewa siku 75 tu, Mwaka huu sitaki kusikia masuala ya upungufu wa vifaa mjipange mapema ili mjue namna ya kutatua changamoto za vifaa".
Kadhalika amesema kuwa wananasiasa ni sehemu ya Mradi huu hivyo amewataka kuwapa ushirikiano wanasiasa wote watakaohitaji kufahamishwa juu ya maendeleo ya mradi, ametaka wasiwaache nyuma wapewe majibu kwa yote watakayohitaji kufahamu.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi Dismas Mwakisambwe amesema kuwa kwa namna yoyote ile lazima Mradi huu utimie hivyo amesena licha ya uchache wa fedha hivyo amewataka kutumia vifaa vilivyobakia wakati wa ujenzi wa madarasa kwa mwaka uliopita ili kuweza kufikia malengo.
Amewataka pia Watendaji, Wakuu wa Shule kuzingatia ushauri wa wataalamu na pale kunapotokea shida yoyote ya kitaalamu basi wasisite kuuliza. Licha ya kuwepo kwa umbali amewataka kutumia hata njia ya simu ili kutatua tatizo hilo kwa haraka zaidi ili kuepusha kupoteza muda.
"Tuepuke njia ya mkato lazima wataalamu wanapotoa ushauri basi muufuate maana hao ndio wanaofahamu mambo hayo, lakini pia lazima tufuate utaratibu tusipendelee kutumia njia ya mikato lazima tufuate utaratibu hata kama itachukua muda".
Kadhalika amewataka kutumia nyaraka na viambatanisho ili kuwepo kwa taarifa kamili ya Utekelezaji wa miradi hiyo kuanzia mwanzo mpaka hatua ya mwisho.
"Ni lazima kuwepo na vitabu vya kupokelea vifaa, vitabu kwa ajili ya kutunzia kumbukumbu, matumizi ya kila siku pamoja na wageni wote wanaohudhuria katika maeneo ya utekelezaji".
Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imepokea kiasi cha Tsh 980,000,000= kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 49 vya madarasa katika shule 23, ndani ya Halmashauri.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa