Kikao kazi kwa watendaji wa elimu ngazi ya Shule, Kata na Halmashauri tarehe 9/9/2022
kuweka mikakati ya kuinua ubora wa elimu.
Kikao hicho ambacho kimefanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Tosamaganga, kilikuwa na dhumuni la kujadili changamoto za kuinua kiwango cha ufaulu. Katika kikao hicho ziliibuka changamoto nyingi ikiwemo ya uhaba wa walimu, umbali kutoka makazi ya watu na shule, utoro wa wanafunzi, wazazi kutokuwa tayari kuchangia chakula pamoja na baadhi ya Walimu hawana ari ya kufanya kazi na kutokaa kwenye vituo vyao vya kazi.
Akiongea kwenye kikao hicho Afisa Elimu Ndugu Sylivester Mwenekitete amesema “Kutokana na kushuka kwa ufaulu sisi kama Watendaji tunatakiwa kuzingatia usimamizi wa ufundishaji, kuanzia maandalizi, kabla ya kwenda kufundisha na kuhakikisha kama Mwalimu anafundisha au hafundishi”, kwani hii itasaidia kila mwalimu kujua wajibu wake”.
Pamoja na hayo Mwenekitete ameoza kusema kuwa, wanafunzi wanatakiwa kufanya mitihani ya mara kwa mara kwa kufuata mpangilio sahihi (format), na matumizi ya lugha ya Kiingereza katika ufundishaji. Pia Mwenekitete amewatia moyo walimu na amewasihi kufanya kazi kwa bidi.
Naye Afisa Utumishi na Utawala Bi. Beatrice Augustine amesema, “kwa upande wa likizo za uzazi ni haki ya kila mtumishi. Kupewa likizo ya uzazi mara baada ya kujifungua, ambapo kwa mtoto mmoja ni siku 84 na watoto wawili ni siku 98, hii ni kwa upande wa wanawake. Pia mwanaume anatakiwa kupewa likizo ya siku tano mara baada ya mke wake kujifungua, ambapo ruhusa hizi/likizo zinatakiwa zianzie kwa Mkuu wa Shule”.
Bi Beatrice ameongeza kusema kuwa, ikiwa imetokea mtoto amefariki baada ya kujifungua mtumishi hatasubiri miaka mitatu ili kupewa likizo nyingine, bali atakaa hadi akipata mtoto mwingine atapewa likizo kama kawaida hata kama ni ndani ya mwaka mmoja tangu alipopata likizo ya uzazi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Wakili Bashir Muhoja ametoa pongezi kwa Walimu kwa kuhudhuria kikao. Pia alitoa ufafanuzi wa changamoto zinazokabili shule mbalimbali ikiwemo kwa Walimu kutokaa katika Vituo vyao vya Kazi kuwa ni tatizo sugu.
Aidha amewaomba Walimu kuweka jitihada katika ufundishaji katika kipindi hiki cha kuelekea mitihani ya mwisho ya Kidato cha Nne, pia Kidato cha Pili, kwani bado wanauwezo wa kufanya vizuri kwa muda uliobaki na kuinua ufaulu.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa