"Msikae Kizembe Kwenye Maeneo yenu ya Kazi" - DC Moyo
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Mohamed Moyo amewataka watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kuepuka kukaa kizembe katika maeneo yao ya kazi na ni muhimu kuchangangamkia fursa zilizopo ili kuwekeza na baadae kuja kuwa msaada wako wakati wa kustaafu.
Ameyazungumza hayo leo tarehe 28.08.2022 alipokuwa akihitimisha Maadhimishi ya wiki ya Utumishi wa Umma kwa Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa yaliyofanyika katika Hospitali Teule ya Wilaya Tosamaganga, ambapo amekuwa Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo.
Amewataka Watumishi wa Umma kuwa na nidhamu ya kazi, kupenda kufanya kazi bila kushurutishwa ikiwemo kuwahudumia wananchi kwa weredi, uzalendo na kwa uaminifu mkubwa bila kutanguliza rushwa au kuchelewa.
Sambamba na hilo amewaomba Watumishi wa Umma kuendelea kupunguza kero za wananchi katika maeneo yao ili kupunguza foleni katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya au Mkoa. Pia amewataka Watumishi wa Umma kuacha kufanya kazi kwa mazoea, wabadilike katika utendaji wao wa kazi.
"Mtumishi lazima uwe mbunifu mahali pa kazi ili hata ikitokea umehamishwa eneo la kazi basi Watumishi na wananchi wakuongelee vizuri kwa kuacha alama na si washangilie na kupika pilau kwa kuondoka kwako".
Mhe. Moyo pia ametoa pongezi kwa Viongozi na Watumishi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwa kufanikisha zoezi la anuani za makazi na hivyo kupelekea kuwa wa kwanza kitaifa ingawa bado zoezi la kuandika na kupachika namba za nyumba linaendelea.
Aidha amesisitiza juu ya upigaji vita masuala ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto, amesema watuhumiwa wote ni vyema kuchukuliwa hatua za kisheria na ni marufuku kwa mtuhumiwa akikamatwa kumalizana wenyewe kwa wenyewe ikibainika pia wote watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Akizungumza katika Maadhimisho hayo Katibu Tawala Wilaya ya Iringa Ndugu Stomin Kyando amesema lengo la maadhimisho hayo ni kukumbushana majukumu ya kiutumishi ambapo amesema kuwa Watumishi wote wa Umma wanafanya kazi kwa ridhaa ya Mhe. Rais kwani yeye ndio mwenye mamlaka ya kuanzisha au kufuta taasisi yoyote nchini.
"Tunapaswa tutekeleze majukumu yetu kwa niaba ya Mhe. Rais, Matendo yako yaakisi na yaendane kama Mtumishi wa Umma, tusifanye dhuluma katika kutoa huduma ni dhambi kubwa, lakini pia ninawashukuru kwa ushirikiano mlionao na kwa kazi mnazozifanya hongereni sana."Amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Wakili Bashir Muhoja amewapongeza Watumishi wote wa Halmashauri kwa ufanyaji kazi mzuri japo kuna baadhi yao ni wakorofi lakini bado anaendelea kuwaelewesha namna nzuri na sahihi ya utendaji kazi kama baba.
Pia amezungumzia suala la mapokezi ya Watumishi wapya wanaotarajia kuwasili na amesema kuwa amewaagiza Watendaji wa Vijiji kuandaa mazingira rafiki kwa Watumishi hao wapya kwa kuwatafutia nyumba nzuri pamoja na mahitaji yao mengine ya msingi kwani kwa kufanya hivyo kutapelekea kuwafanya wajihisi vizuri na wasione tofauti yoyote.
Akisoma risala (Taarifa) ya Maadhimisho hayo Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu Bibi Beatrice Augustino amesema kuwa Halmashauri ina jumla ya Watumishi 3134 na katika maadhimisho haya Jumla ya Kata 8 na Watumishi 226 wametembelewa na mada mbalimbali zimewasilishwa na kulikuwa na jumla ya changamoto 47, changamoto 42 zimetolewa ufafanuzi na changamoto 5 zinafanyiwa uchunguzi.
Tumefanya hitimisho leo kwa kufanya usafi katika maeneo ya Hospitali ya Tosamaganga ninawashukuru Watumishi wote kwa ushirikiano mlionipa na wale Watumishi ambao wametkka nje ya Halmashauri ambao tumezunguka pamoja katika maadhimisho haya ninasema asante na Mwenyezi Mungu awabariki sana.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa