Lyra In Africa Yang’aa Iringa DC
Shirika la Lyra In Africa ni wadau wakubwa wa elimu hapa Mkoani Iringa katika nyanja ya ujenzi wa mabweni (Hostels) kwenye shule za sekondari. Ujenzi huo umelenga kwa ajili ya watoto wa kike ambao wanakabiliwa na changamoto mbambali na kushindwa kutimiza ndoto zao.
Akiongea na Shirika hilo la Lyra Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mheshimiwa Halima Dendego alipokuwa ametembela Shule ya Sekondari ya Ilambilole ambako Lyra wamejenga bweni la wasichana na kuleta vinakilishi 11 (computer) na kisima cha maji amesema, “pamoja na shukrani nyingi ninazozitoa kwenu Lyra, pia nitatoa ushirikiano kwa 100%. Ujenzi wa mabweni mnaojenga katika shule mbalimbali umekuwa ni ukombozi kwa watoto wa kike, na kuwafanya kuepukana na mimba za utotoni, changamoto mbalimbali na umbali mrefu kutoka nyumbani hadi shuleni”
Mheshimiwa Dendego ameendelea kusema, tangu tupate uhuru miaka mingi iliyopita Tanzania ilikuwa na shule chache, ambapo ilipelekea kuchaguliwa watoto wachache na wengine kuishia mtaani kwa kukosa nafasi ya kuendelea na shule. Sasa hivi Tanzania imepiga hatua kubwa sana katika Sekta ya Elimu kwa kufanya mabadiliko na kuweka kila Kijiji shule ya Msingi na kila Kata shule ya Sekondari ili kufanya watoto waendelee na masomo”.
Mheshimiwa Dendego ameahidi kutoa ushirkiano kwa kila jambo watakalofanya Shirika la Lyra katika Mkoa wa Iringa na hasa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa na kumuagiza Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Iringa Wakili Bashir Muhoja ahakikishe Shirika la Lyra wanafanya kazi zao bila usumbufu wowote.
Naye Diwani wa Kata ya Kising’a Mheshimiwa Ritha Mlagala amesema, “tunawashukuru Shirika la Lyra in Africa kwa msaada wao wa kujenga bweni, vinakilishi na kuchimba kisima, kwani sasa hivi watoto hawapati changamoto za mimba wala kuishi katika mazingira magumu”.
Shule ya Sekondari Ilambilole ina watoto wa kike zaidi ya 280, na kumshukuru Mkurugenzi Mtendaji Wilaya kwa kuwatia moyo wa kuendelea kupambana.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Iringa Wakili Muhoja amesema, “ombi langu ni kuwa Mhandisi wa Miundombinu awe anakuja kila mara kukagua ujenzi unaoendelea ili kutoa ushirikiano mzuri kati ya Wadau hawa na Halmashauri”. Pamoja na kujenga bweni Shule ya Sekondari Ilambilole Lyra wamejenga mabweni mengine shule ya Sekondari Nyang’oro na Mseke, amesema Wakili Muhoja.
Wakili Muhoja ameendelea kusema kuwa, atahitajika Mwalimu wa kuwafundisha watoto kinakilishi (Computer) ili wapate kujifunza vizuri, na kuomba vinakilishi hivi vitunzwe vizuri na kwa usafi.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Lyra Bibi. Maria ametoa shukrani kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, kwa kutenga muda wake kuwapokea na kuwasikiliza. Lyra wanaahidi kutoa ushirikiano na kuwa karibu na Halmashari ya Wilaya ya Iringa.
Akitoa shukrani zake kwa Lyra Mkuu wa Shule ya Sekondari Ilambilole Mwl. Elda Myenzi amesema, sasa hivi wameweza kupandisha ufaulu kutokana na watoto kuishi bwenini kwani wanapata muda mzuri wa kujisomea ambapo kuna mazingira rafiki ya kujifunzia.
Pamoja na mafanikio hayo Mkuu wa shule amebainisha changamoto zinazoikabili shule hiyo ambazo ni vinakilishi vichache na mfumo wa choo siyo rafiki.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa