"Ifanye kazi yako kuwa sehemu ya Ibada"- Mkuu wa Idara Utumishi Beatrice Augustino
Ifanye kazi yako kuwa sehemu ya ibada, tutekeleze kazi zetu kwa uadalifu mkubwa, tukifanya hvyo ndivyo tunavyobarikiwa sisi, na familia zetu, tuzitendee haki ipasavyo kazi tunazozifanya.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mkuu wa Idara ya Utumishi Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Bi Beatrice Augustino ameyasema hayo katika uzinduzi wa Maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2022.
Maadhimisho hayo yamefunguliwa rasmi leo tarehe 23, Juni 2022 katika Kata ya Wasa na kukutanisha baadhi ya watumishi kutoka kata hiyo wakiongozwa na Mtendaji wa kata ya Wasa Ndugu Daudi Mohamedi, Watendaji wa Vijiji, baadhi ya Walimu kutoka shule za Msingi na Sekondari, Maafisa Kilimo pamoja na wataalamu wa Afya.
Akizungumza katika maadhimisho hayo Kaimu Mkurugenzi Bi Beatrice amesema Ofisi ya Rais, Menejinenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ni Mratibu wa maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma nchini na maadhimisho haya ni moja ya matukio katika kalenda ya Umoja wa Afrika (AU) ambapo nchi wananchama huadhimisha kwa kufanya maonesho ya kazi mbalimbali na kongamano kuhusu masuala ya Utumishi wa Umma.
Aidha Amesema kuwa chimbuko la maadhimisho haya ni uamuzi wa Mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya Utumishi wa Umma uliofanyika Tangiers, Nchini Morocco mwkaa 1994, Uamuzi huu ulizitaka nchi za Afrika kusheherekea wiki hii kwa kauli mbiu moja kwa Bara zima la Afrika."Kauli mbiu ya Maadhimisho haya kwa mwaka 2022 ni Kuimarisha Ustahimilivu wa Utawala wa Umma katika Afrika ili kuwezesha utambuzi wa Mahitaji ya Lishe Afrika wakati na baada ya Janga la Corona".
Kauli mbiu ndogo ambayo imependekezwa kutumika kwa nchi yetu ni "Ni nafasi ya Mapinduzi ya Nne ya Viwanda katika masuala mapya yanayojitokeza kuhusu utoaji wa huduma na urejeshaji wakati na baada ya janga la corona.
Kadhalika amesema kwa mwaka 2022, Maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma yataadhimishwa kwa kuwatembelea watumishi na watendaji wa Taasisi za Umma walio katika maeneo ya pembezoni ili kuhimiza uwajibikaji wa hiari, kusikiliza changamoto zinazowakabili kiutendaji na kuzitatua.
Pia ameishukuru pia Serikali ya awamu ya sita kwa kufanya kazi nzuri, ndani ya mwaka mmoja wa awamu hiyo Halmashauri ya Wilaya ya Iringa pekee watumishi 1700 wamepandishwa vyeo, pia kwa mwaka huu wa fedha 2021/2022 malimbikizo mbalimbali ya mishahara tangu 2017 kwa takriban watumishi 500 wamelipwa kiasi cha Tsh. Biln 01.
"Tunamshukuru mama na Serikali kiujumla kwa jitihada na juhudi zao walizozionesha kwa Watumishi wa Umma, lakini pia tunamshukuru kwa jambo la mama ambalo kwa wengi wetu tunalisubiri kwa hamu pale mwezi wa saba".
Ushauri wangu, ninajua kuwa Watumishi wengi hapa lengo lao ni kufanya majazilizo ma kabla ya kufanya hivyo basi ninawashauri ni lazima uwe na mipango, kitu cha kwanza ni mipango halafu ndio kujaziliza, ikiwa kujaziliza itakuwa ya kwanza hatutafanikiwa, maana ukishapata pesa matatizo yanakuja, kwa hyo nasisitiza mipango kwanza halafu ndio mengine yafuate. Ameongeza.
Amesema haki na wajibu vinaenda sambamba, madaraja, kima cha chini, madeni tumelipwa hivyo tufanye kazi kwa haki na wajibu."Kama unafikiri kazi hauielewi basi ni vyema kuuliza kwa watu sahihi, una changamoto uliza, maswali mengine ni mepesi sana ilaa tunapewa majibu magumu hivyo tuwasiliane kwanza". Amesisitiza.
Akizungumza katika Maadhimisho hayo Afisa TAKUKURU Mkoa Ndugu Ditram Muhoma amesisitiza juu ya suala la uadilifu kwa Watumishi na amewataka kutenda jambo bila kuambiwa au kusukumwa na kila mmoja atimize wajibu wake mahala pa kazi.
Akizungumza Kuhusu athari na madhara ya Rushwa kiutumishi amesema ni pamoja na kuwa na Watumishi wasiowajibika, wasio na sifa kutokana na masuala ya kutoa hongo ili kupata nafasi fulani na mwisho wa siku kupata watumishi amabao ni wabovu, lakini pia ni kupelekea kukosekana kwa fursa sawa kwa wote kutokana na wachache wao kupita mlango usio stahili, kubwa kuliko amesema kuwa ni kudhalilisha Utumishi wa Umma.
Ili kuepukana na hizi athari Ndugu Muhoma amesema watumishi wanatakiwa kuwa waadilifi, wenye staha, wachapa kazi wasiopendelea, wawazi, kuwa na utaratibu wa kupokea maoni pamoja na malalamiko kutoka kwa wananchi ambao ndio wateja wetu.
Akizungumza katika maadhimisho hayo Mwanasheria wa Halmashauri Method Msokele amesema kuwa watumishi wengi wamekata tamaa kutokana na Watumishi wenyewe kutokujituma, kutokuwajibika kwa sheria pamoja na kuwepo kwa malalamiko ya kutokupandishwa vyeo.
"Tunatakiwa tuwe waaminifu, wawajibikaji kwa kuzingatia sheria na bila kuvuka mipaka, tuwe wawazi katika shughuli zetu za kiutumishi aidha tuwe waadilifu na tuwe huru."
Wakitoa changamoto mbalimbali na kero katika Maadhimisho haya baadhi wa Watumishi wametoa madai yao kama vile masuala ya kucheleweshewa mafao mbalimbali, uhaba wa watumishi katika Idara mbalimbali, uhamisho wa Watumishi, Malipo ya fedha za kujikimu kwa Watumishi, kadi za utambulisho wa Watumishi, Ubovu wa miundombinu pamoja na changamoto za TEHAMA.
Changamoto na kero zote zimetolewa majibu na Wataalamu walioongozana na Kaimu Mkurugenzi Bi Beatrice Augustino lakini pia zingine zimechukuliwa kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
Maadhimisho haya yameanza leo terehe 23.06 2022 na kutamatishwa tarehe 28.06.2022, yanatarajiwa kuendelea kuadhimishwa katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ikiwemo Idodi, Pawaga, pamoja na Kalenga.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa