Makatibu Tarafa, Watendaji wa Kata, Vijiji na Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Kata Wanolewa Ukusanyaji Mapato
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Wakili Bashir Muhoja akiwa na Kamati ya Menejimenti ya Halmashauri hiyo, amekutana na Maafisa wote wa Tarafa na Kata kwa ajili ya kuweka mikakati ya ukusanyaji mapato tarehe 03/11/2022.
“Kama Kamati ya Menejimenti ya Halmashauri hii tumekubaliana tukae pamoja na kupeana maelekezo ya namna ya kuendesha Halmashauri. Katika mambo makubwa yanayotakiwa kufanyika ni ukusanyaji wa mapato na kusimamia miradi ya maendeleo, na kwamba jambo hili liwe na uelewa wa pamoja. Kila Afisa kwa anatakiwa kusimamia ukusanyaji mapato katika eneo lake na kwa uaminifu sana, kwani Halmashauri inategemea sana ukusanyaji wa mapato katika uendeshaji wake”. Haya yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa wakati akiongea na Maafisa hao Ngazi ya Tarafa na Kata.
Sambamba na hilo Wakili Muhoja amewaambia Maafisa hao kuwa, wana mpango wa kupita kila Kata kwa siku tatu mfululizo, kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo. “Tumeandaa mpango wa kupita kila Kata kutembelea na kukagua miradi inayoendelea. Hivyo muda ukifika tutapeana taarifa ili kila mmoja wenu ajiandae na kutoa taarifa kamili ya maendeleo ya mradi katika eneo lake, na kwamba siku ya Baraza la Madiwani itatakiwa kutolea taarifa ya kila mradi.”
Wakili Muhoja ameendelea kuwaasa Maafisa hao kuwa, waache tabia ya kujisemesha kwa wananchi kuwa ndiyo wameleta maendeleo ya ujenzi miradi inayoendelea. “mnajisema kwa wananchi kuwa ninyi mmeleta fedha kwa juhudi zenu, mimi kama Mkurugenzi wa Halmashauri sipendi unafiki wala majungu. Iwapo fedha za miradi zimefika nje ya bajeti huwa natoa taarifa kwa Waheshimiwa Madiwani ili kila mmoja wetu afahamu jambo hilo. Lakni Mtendaji anapojisifia kuwa yeye ndiye kaleta fedha za miradi unakuwa ni unafiki jambo ambalo halina afya kwa ustawi wa Halmashauri”.
Wakili Muhoja ameendelea kuwaambia Watendaji wa Kata kuwa, Walezi wa Kata watakapopita kwenye Kata wanatakiwa kutoa ushirikiano na kueleza uhalisia wa maendeleo ya Kata, hakuna haja ya kificho kwani hali halisi inajulikana.
Wakili Muhoja amewaasa Watendaji kutoa elimu kwa wananchi kutokana na uchumi na hali ya chakula. “Wananchi wasijisahau kuuza chakula hadi wakaishiwa, kwani hali siyo nzuri, lazima kuwepo na chakula cha akiba”
Ameongeza kusema kuwa, uandikishaji wa mbolea ya ruzuku ufuate sheria na haki bila kufanya upendeleo.
Kwa upande wa Maafisa Ngazi ya Kata nao walitoa changamoto zao, na Mkurugenzi Mtendaji amezichukua kwa ajili ya kuzifanyia kazi.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa