Kama ilivyo Sheria na Kanuni za Tanzania, kila baada ya miaka mitano kunakuwa na Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani kwa ajili ya kuongoza Serikali, na kwamba Uongozi uliopo madarakani kwa wakati huo hukoma madaraka yao.
Juni 19, 2025 Mkutano wa Baraza la Madiwani ulifanyika ili kuvunja Baraza na kwenda kujiandaa kwa ajili ya kugombea tena kwenye maeneo yao kwa nia ya kuwepo madarakani.
“Usilipe Kisasi, Mwachie Mungu, kuna wakati tunatamani mambo yetu yawe mazuri lakini Mungu anapanga yake hivyo tuombeane mema.
Kuna kipindi tulipitia wakati mgumu sana na tulilia sana lakini mimi kama Kiongozi nililia kimya kimya zaidi yenu”. Hayo ni baadhi ya maneno mazito aliyotoa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mhe. Stephen Mhapa alipokuwa anatoa hotuba katika Mkutano wa Baraza la Madiwani wa Kuvunja Baraza la Mwaka 2024/2025.
Mhe. Mhapa ameongeza kusema kuwa, “nawapenda Watumishi, hivyo tuombeane ili tuweze kufika mahali kwa pamoja, na mtambue kuwa, nilipokuwa Mwenyekiti nilikuwa ni Kiongozi, Baba na Mlezi”.
Aidha, Mhe. Mhapa amesema anamshukuu Mhe. Rais kwa kuleta fedha za miradi, ambapo sasa hivi wanaweza kujivunia na kusemea mbele ya wananchi.
Mhe. Mhapa amewatakia heri, Madiwani na Watumishi na kuomba kuendelea kujuliana hali na kupeana maarifa.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Iringa amewaasa Madiwani kuwa, baada ya kuvunjwa kwa Baraza wao watakuwa Wanachama tu, na kuwaomba wasijihusishe katika vitendo vya utoaji na kupokea rushwa wakati wa mchakato wote wa uchaguzi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Ndugu Robert Masunya amesema, ana faraja ya kuwa na Baraza hili tangu alipoteuliwa na Mhe. Rais kuongoza Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kama Mkurugenzi.
Ndugu Masunya amewaambia Madiwani kuwa, wanapoondoka kwenda likizo wanaiacha Halmashauri ikiwa katika mikono salama chini ya Uongozi wake, na kwamba wamefanya Halmashauri kwa Utatu ambao ni Uongozi, Ulezi na Uvumilivu.
Ndugu Masunya ameahidi kuwa, yale yote yaliyoagizwa na Madiwani atayasimamia na kuyatekeleza kama walivyoagiza, na kwamba yupo tayari kwenda kuwasemea mazuri kwa wananchi katika maeneo yao.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa