Mapambano Dhidi ya UVIKO 19 Yanaendelea Halmashauri ya Wilaya ya Iringa
Halmashauri ya Wilaya ya Iringa inaendelea na zoezi la uchanjaji chanjo yza UVIKO 19, hadi sasa imefanikiwa kwa 61% na kwamba inatakiwa ifike 70% kwa maelekezo ya awali ya Serikali, na kutolewa maelekezo mengine kuwa ni lazima ifike 100%.
Akifungua kikao kifupi kilichohusisha Watendaji wa Kata wa Jimbo la Isimani, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Daktari Samwel Marwa amesema “kwa sasa tumepata Mdau mwingine ambaye ataweza kudhamini zoezi la uendelezaji wa uchanjaji. Mdau huyo ni Benjamin Mkapa Foundation ambayo itasaidia zoezi hili. Katika Tanzania ni Mikoa 10 tu na Halmashauri 24 zimechaguliwa kupewa usaidizi huu, Mkoa wa Iringa tumepata bahati hii, na kwamba Halmashauri tatu zikiwa ni Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Mufindi na Kilolo. Hivyo tutumie fursa hii vizuri kwani tumeongezewa nguvu sana”, amesema Dkt Marwa.
Jambo hili limetokana na kuona kuwa, Mkoa wa Iringa upo nyuma sana kitakwimu katika uchanjaji hasa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, hivyo Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation kuona umuhimu na kuleta mchango wao.
Akitoa ufafanuzi wa jinsi ya zoezi hili litakavyoenda Mratibu wa Chanjo wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation Ndugu Clarence Mkoba amesema, “Taasisi imepata pesa hii ili kusaidia Mikoa hiyo kumi ikiwemo na Iringa. Hivyo Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imeonekana kuwa zoezi la uchanjaji lipo chini sana ukilinganisha na maeneo mengine”
Ndugu Mkoba ameongeza kusema kuwa, “Tumekaa na Kamati ya Afya Mkoa kuona namna ya kuliweka sawa zoezi hili ili lifanikiwe kwa ufanisi, ndipo tukaona tuonane na Watendaji wa Kata husika ili tupeane maelekezo.”
Akitoa mikakati ya jinsi kazi ya uchanjaji itakavyofanyika, Ndugu Mkoba amesema “Mpango ni kuchanja nyumba kwa nyumba, na kwa kutumia mikutano ya kijamii, ili tufikie lengo la 100% tuliyojiwekea. Pia taarifa hiyo inatakiwa kuingizwa kwenye mfumo kila siku wakati zoezi linatekelezwa na kwamba kiwango cha takwimu kiongezeke hadi 95%”, kwani tumepangiwa siku tisa tu za kazi hii”, amesema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Mohamed Moyo, amewaambia Watendaji hao kwa kusisitiza juu ya jambo hili kuwa, kama hali halisi inaonekana basi si vizuri kukaa kimya, taarifa itolewe kwa usahihi ili kujua ukweli. Pia Watendaji watumie makundi ya michezo na mikutano ya wananchi kuhamasisha uchanjaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Wakili Bashir Muhoja ametoa shukrani kwa msaada huo ili kuongeza nguvu katika hili. Pia atatoa ushirikiano kwa kila hatua ili kufanikisha zoezi hili.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa