MBOMIPA Kung’ara Tena
Elimu imeendelea kutolewa juu ya Uhifadhi wa Matumizi Bora ya Maliasili kwa Idodi na Pawaga (MBOMIPA) na Maeneo ya Jamii ya Hifadhi ya Wanyamapori (Wildlife Management Area – WMA) kwenye vijiji vinavyozunguka Mbuga ya Wanyama ya Ruaha, ambapo Wadau wa Mashirika ya Lion Landscape na STEPS wameweza kutoa elimu hiyo kuanzia shule za Msingi na Sekondari katika vijiji vya Tarafa ya Pawaga na Idodi.
Sambamba na utoaji elimu kwa wanafunzi pia wameweza kutoa elimu kwa jamii kwa kuanzisha mashindano ya michezo kwa kugombea zawadi na Makombe ikiwa ni njia nyingine ya kutoa elimu.
Akiongea katika ufunguzi wa mashindano hayo Mkuu wa Kitengo cha Maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Bi. Fatuma Juma amesema, “pamoja na kutoa elimu juu ya uhifadhi wa maliasili na mazingira, pia michezo ni afya. Michezo hii inahamasisha jamii kushirikiana na kujenga uelewa wa pamoja juu ya uhifadhi”.
Akiongea na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mratibu wa Mashindano hayo Ndugu Wiston Mtandamo amesema, “mashindano haya yanachochea uelewa wa namna ya kuishi na wanyama pori ambao ni rasilimali za Taifa letu. Pia inaongea uelewa wa kuepukana na mambo ya ujangiri katika kuwawinda au kuwaua wanyama pori na uhifadhi wa mazingira kwa ujumla”.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Uhifadhi wa Maliasili na Wanyamapori Ndugu Jonas Mkusa amesema, “nawapongeza Wadau wa MBOMIPA kwa kuanzisha mashindano haya na kwamba hii itachochea umuhimu wa uhifadhi katika jamii, na kutokomeza shughuli za ujangiri na uwindaji haramu”.
Mechi ya ufunguzi ilikuwa kati ya timu ya Malinzanga ya Kata ya Mlowa Kijiji cha Mlowa na timu ya Magombwe ya Kata ya Mlenge Kijiji cha Magombwe, ambapo mshindi alipatikana timu ya Magombwe kwa mikwaju ya penati.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa