Mhapa Awataka Watendaji kutoa Ushirikiano kwa Madiwani
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mhe. Stephen Muhapa amewataka Watendaji Kata Kutoa ushirikiano kwa Madiwani ikiwemo kuwataarifu kuhusu maagizo wanayoyapata na Miradi inayokwenda kutekelezwa katika Kata husika.
Ameyasema hayo katika Mkutano wa Baraza la Madiwani wa Robo ya kwanza uliofanyika tarehe 09-10/11/2022 katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo, amesema katika utekelezaji wa miradi lazima kuwepo na ushirikiano baina ya Watendaji na Madiwani hivyo utoaji wa taarifa itasaidia kuboresha na kuchochea ukamilikaji wa miradi.
Pia amesema kuwa waheshimiwa Madiwani wana nafasi kubwa katika maendeleo ya Halmashauri hivyo wanapaswa kuzungumza na kujenga hoja zenye mashiko kwa Halmashauri.
Kadhalika amewata waheshimiwa Madiwani kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu na wataalamu kutoka Halmashauri kwani Taasisi hiyo inajengwa na pande zote mbili yaani Baraza la Madiwani na Wataalamu hivyo ushirikiano ndio chachu ya maendeleo.
“… Hata shilingi ina pande mbili na ukitoa upande mmoja haitakua na thamani yoyote ndivyo hata sisi yatupasa tuwe, tufanye kazi kwa pamoja na kwa kushirikiana baina yetu sisi Madiwani na Wataalamu wetu.”
Aidha Waheshimiwa Madiwani wamewasilisha taarifa za Kamati za kudumu za Halmashauri na taarifa za utekelezaji wa Kata kwa kuwasilisha changamoto walizokumbana nazo kwa robo ya kwanza, miongoni mwa changamoto nyingi zilizowasilishwa ni Uhaba wa Watendaji wa Vijiji, Uhaba wa nyumba za Waalimu, na upungufu wa waalimu pamoja na uchakavu wa miundombinu.
Akijibu hoja hizo Mwenyekiti wa Halmashauri amewataka Waheshimiwa Madiwani kuendelea kusubiri wakati changamoto hizo zikiendelea kutatuliwa, Hapa kinachotakiwa ni uwezo wetu wa kibajeti kama bajeti yetu itaruhusu basi tutaangalia namna ya kutatua changamoto hizi na hatuwezi kuzitatua kwa mara moja tutaangalia tumepata kipi na tupeleke wapi. Amesema.
Naye Mbunge wa Jimbo la Ismani Mhe William Lukuvi ameshauri na kusema kuwa Waheshimiwa Madiwani wana nafasi ya kukutana na kujadili kuhusu upandishaji wa ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri kwa kufanya vikao na kuja na hoja za ni kwa namna gani tunaweza kupandisha ukusanyaji wa mapato yetu ili hata hizi chagamoto zetu tuweze kuzitatua kwa fedha zetu za ndani.
“kadri tutakavyokua tumekusanya mapato kwa kiasi kikubwa ndivyo tutakavoweza pia kupunguza uchangishaji kwa wananchi na tutakuwa na uwezo wa kukamilisha miradi hiyo sisi wenyewe.”
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Wakili Bashir Muhoja amewashukuru Madiwani kwa kuchangia hoja zenye mashiko kwa Halmashauri na kuwaomba watoe ushirikiano katika Miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Kata zao ikiwemo Miradi ya ujenzi wa madarasa ya kidato cha kwanza 2023.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Iringa Vijijini Mhe. Costantino Kiwele amesema kuwa anawapongeza Halmashauri kwa kuendelea kuratibu na kusimamia zoezi la utoaji wa chakula kwa wanafunzi mashuleni kwani ni ajenda ya kitaifa.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa