DC Moyo azindua zoezi la Upandaji Miti Halmasahuri ya Wilaya ya Iringa
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Mohamed Hassan Moyo amezindua zoezi la upandaji miti ambalo limefanyika katika Tarafa ya Mlolo, Kata ya Masaka, Kijiji cha Sadani eneo la Shule ya Sekondari Mseke tarehe 03/03/2022.
Akizindua zoezi hilo Mheshimiwa Moyo amesema, miti takribani mia moja imepandwa katika eneo hilo, huku Kauli Mbiu ya Mwaka Huu ni : "Miti Mazingira Yangu, Tanzania Yangu, Naipenda Daima", ambapo inakadiriwa kupandwa miti milioni moja na laki tano kila mwaka.
Katika hotuba yake Mheshimiwa Moyo amefurahishwa na mahudhurio ya wananchi kwa kushiriki uzinduzi huo, amesema “Mkusanyiko huu wa wananchi unaonesha wazi kuwa, mmejidhatiti katika shughuli hii ya upandaji miti”.
Aliongeza kusema kuwa malengo ni kupanda miti milioni moja na laki tano kila mwaka, hii itasaidia kuboresha hali ya hewa na wananchi kujikwamua kiuchumi kutokana na shughuli hii ya ulimaji miti.
“Upandaji wa miti ulishaanza na utaendelea hadi mvua zitakapokoma”.
Ili kuboresha kilimo cha miti ni lazima kuzingatia kupalilia, kulinda miti, kuzuia moto, pia kuwa wavumilivu ili kuvuna baada ya muda uliopangwa kitaalamu, amesisitiza.
Wakati huohuo Mh. Moyo ametoa maagizo kwa wananchi kuwa, kuna wafanyabiashara ambao si waaminifu wanauza mbolea ambayo si halisi, na kupelekea kuwadanganya wananchi. Amewataka wananchi kutoa taarifa kwa viongozi wa Serikali au Polisi mara wanapobaini kuna mtu wa namna hiyo.
Lakini pia ametoa msisitizo kwa wananchi kutoa ushirikiano katika suala zima la anuani za makazi, Sensa ya Watu na Makazi, pamoja ugonjwa wa UVIKO – 19 ili watu wakapate chanjo, kwani zinapatikana bure katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Ponsiano Kayage amewapongeza wananchi wa Kata ya Masaka kwa kukubali kufanyika uzinduzi katika eneo lao, na kuwataka kuwa mfano wa Kata zingine katika shughuli ya upandaji miti.
“Miti ni uhai wa viumbe vyote duniani, hivyo madhara ya ukataji miti tunatambua. Yatupasa kuwajibika kupanda miti kila wakati”, amesema.
Naye Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Bi. Lucy Nyallu amempongeza na kumshukuru Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Moyo kwa kukubali kuwa Mgeni Rasmi katika zoezi hili la uzinduzi wa upandaji miti.
Aidha amesema kuwa, zoezi hili lilianza kufanyika mapenda mwaka huu na leo ilikuwa ni siku ya uzinduzi tu, na kwamba zoezi hili litakuwa endelevu.
Akitoa taarifa ya uzinduzi wa upandaji miti Afisa Misitu wa Wilaya Ndugu. Joachim Mshana amesema, shughuli ya upandaji miti hufanyika kila tarehe 1/04, lakini katika ngazi ya Halmashauri imeadhimishwa leo tarehe 03/03/2022.
“Katika miaka mitano iliyopita ilipandwa miti 10,367,967 lakini miti ilipona na kukua vizuri ni 6,682,000 sawa na 49%.”
Pia Ndugu Mshana amewashukuru wadau mbalimbali kwa michango yao katika kufanikisha shughuli hii ya upandaji miti wakiwemo, Mfuko wa Misitu Tanzania (TAFF), Wakala wa Huduma za Misitu(TFS), One Acre Fund, Clino Development Initiative, world vision, Forest Development Trust na Panda Miti Kibiashara.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa