Milioni 128 Kujenga Mradi wa Shamba Darasa Kilimo cha Samaki Ibumila
Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imepokea fedha kiasi cha shilingi Milioni mia moja ishirini na nane (128) kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa lengo la ujenzi wa shamba darasa la kujifunzia namna ya ufugaji wa samaki katika Halmashauri.
Akizungumza katika utambulisho wa mradi huo ambao utatekelezwa katika Kijiji cha Ibumila Kata ya Mgama Mkuu wa Idara ya Ujenzi Mhandisi Nicco Kasiririka amesema mradi huo umefadhiliwa na Wizara na utatekelezwa kwa muda wa miezi mitatu.
Mhandisi Kasisirika amesema mradi huo utahusisha ushiriki wa nguvu za wananchi na kwa wakati huu itakua tofauti na miradi mingine, kwa mradi huo amesema wananchi watalipwa na wao watatoa nguvu kazi katika uchimbaji na ufanyaji kazi
“Tutakua tumezalisha ajira, na tunategema wananchi wajitokeze kwa wingi kuchangamkia fursa hii kwani kazi kubwa itakua ni kuchimba mabwawa na kusaidia katika shughuli za ujenzi”
Aidha Mhandisi Kasisirika amesema utaandaliwa utaratibu mzuri wa malipo kwa wananchi na kuwatoa hofu kuwa hakutakuwa na changamoto yoyote kwani fedha zipo tayari.
Naye Msimamizi wa Sekta ya Uvuvi Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Kelvin Ndege amesema mradi huu utahusisha ujenzi wa Mabwawa manne, Ofisi ya Afisa Uvuvi, choo, chumba cha darasa na uzio.
Amesema lengo la mradi huo ni kukuza uchumi kwa wananchi na kuongeza kipato kupitia shughuli ya ufugaji wa samaki lakini pia amesema shamba darasa hilo litatumika kama sehemu rasmi ya mafunzo kwa Halmashauri nzima na Mkoa kiujumla.
“Tukiangalia Iringa yetu katika nafasi ya kitaifa inashika namba nne kwa udumavu na hii inatokana na ukosefu wa lishe bora, tunatarajia kupitia shamba darasa hili la ufugaji wa samaki litawanufaisha wanakijiji cha Ibumila na Halmashauri kiujumla kwa kupata lishe bora na elimu ya lishe.”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Ibimila Mhe. Richard Mhema ameshukuru kupelekwa kwa mradi huo katika Kijiji cha Ibumila na kuahidi kuwa kama kijiji watatoa ushirikiano na wataunda kamati za utunzwaji na uendelezaji wa mradi huo.
Mradi wa shamba darasa kilimo cha samaki unatarajiwa kuanza hivi karibuni mara baada ya kuundwa kamati mbalimbali za usimamizi.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa