Mkurugenzi Iringa DC Awataka Watumishi Kuepuka Mikopo ya Mitaani
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Wakili Bahir Muhoja amewataka watumishi kuwa makini na mikopo ya mitaani ambayo ina riba kubwa kuliko hata mkopo wenyewe.
Wakili Muhoja ameyasema hayo mapema leo tarehe 02, Januari 2023 alipofanya kikao na watumishi wa Halmashauri kwa robo ya pili mwaka wa fedha 2022/2023 kujadili utendaji kazi, kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Halmashauri (Siasa ni Kilimo).
Amesema watumishi walioomba mikopo hadi sasa ni 88 na fedha iliyokuja kwa ajili ya kukopesha watumishi ni milioni 300 na jumla ya kiasi kilichoombwa ni Bilioni 1.68 hivyo kuna baadhi waombaji itabidi wakose
Katika kikao hicho mada mbalimbali zimewasilishwa ikiwemo Malezi ya Watoto na unyanyasaji wa kijinsia pamoja na Lishe. Akiwasilisha mada ya unyanyasaji wa kijinsia Afisa Ustawi wa Jamii Bibi Gladness Amulike amewataka watumishi kukataa kutumika ili kupata wepesi katika jambo fulani mathalani cheo au madaraka.
“Wewe kama Mtumishi usikubali kutumika kufanya mapenzi kazini ili usaidiwe huo ni udhalilishaji, lakini pia msikubali kushikwa sehemu zisizofaa na wakuu wa kazi”.
Kadhalika amesema kuwa ili kuzuia ukatili mahala pa kazi inabidi mtumishi anapoona kuna dalili za ukatili atoe taarifa (katika Idara ya Utawala au Dawati la malalamiko (Afisa Kero), lakini pia kuwepo na elimu ya mara kwa mara kwa watumishi kuhusu ukatili mahali pa kazi.
Naye Afisa Lishe wa Halmashauri Bibi Tiliza Mbulla amewataka watumishi kuzingatia ulaji sahihi wa chakula kwani chakula kina virutubisho ambavyo vinasaidia kuzalisha nishati kwa ajili ya mwili ikiwemo ukuaji na kuendesha mifumo ya uzazi.
“Hali ya kiafya inatokana na ulaji wa mtu hivyo hali inaweza kuwa mbaya au nzuri kutokana na ulaji wa mtu husika”.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmasahuri Wakili Muhoja amesema ni lazima kwa watumishi kujali afya zao wakiwa maeneo ya kazi lakini pia ni alzima kujali utu wa watumishi na familia zao kwani mtumishi akiwa mgonjwa basi hawezi kufanya kazi kwa ufasaha.
Aidha amewapongeza watumishi kwa kazi nzuri katika nyanja zote amesema tumeanza mwaka vizuri na anatumaini watafanya vizuri zaidi.
“Ukusanyaji wa mapato umeshuka hivyo tujitahidi kukusanya mapato vizuri, kadhalika madeni na stahiki za watumishi zilipwe lakini kubwa zaidi ni nidhamu hasa kwa viongozi na wakuu wa kazi ikiwemo kuwepo kazini, kufanya kazi na kupokea maelekezo.”
Pia Wakili Muhoja amelizungumzia suala la maandalizi ya kuhamia Makao makuu ya Halmashauri yaliyojengwa katika Kijiji cha Ihemi Kata ya ifunda amesema ujenzi unaendelea kukamilika na bado ujenzi wa ukuta ambapo hadi kufikia mwezi aprili tutakuwa tumeshahamia na kuhusu samani zitanunuliwa.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa