Siku Tatu za TASAF Iringa DC Kuwapa Madini Wawezeshaji kuhusu Warsha za Jamii
Na Ofisi ya Habari na Uhusiano Iringa DC
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Wakili Bashir Muhoja amefanya ufunguzi wa mafunzo ya kujenga uelewa kuhusu uendeshaji wa warsha za jamii, Ufanisi wa zoezi la malipo, Masharti ya Elimu/Afya na majukumu ya usimamzi kamati ya usimamizi CMC.
Ufunguzi huo umefanyika katika Ukumbi wa Ofisi za Mipango zilizopo katika Jengo la Siasa ni Kilimo ambapo mafunzo hayo yatadumu kwa muda wa siku tatu kuanzia tarehe 10 hadi tarehe 12 Mwezi Mei 2022.
Katika ufunguzi huo Mkurugenzi Mtendaji Wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Wakili Bashir Muhoja ambaye amekuwa Mgeni rasmi wa ufunguzi huo ameshukuru uongozi wa TASAF kwa kumpa fursa hiyo na kumfanya kujumuika pamoja katika ufunguzi huo.
Amesema warsha za jamii ni mikutano inayoandaliwa na kufanyika ili kuwajengea walengwa wa mpango uelewa wa mada muhimu zitakazosaidia kubadaili mtazamo na fikra kwa nia ya kujiletea maendeleo.
"Uwepo wa warsha za jamii zitatumika kuhusisha taarifa za kaya na walengwa kutoa na kubadilisha mawazo na uzoefu. Maafisa ugani waliopo ngazi ya kata ndio wanajukumu la kuendesha warsha za jamii".
Kuhusu ukosefu wa elimu miongoni mwa walengwa juu ya warsha hizi na ufanisi wa zoezi la malipo na masharti ya elimu na afya Mkurugenzi amesema;
"Ndugu washiriki elimu kwa walengwa inabidi itolewe kila wakati na wawezeshaji wetu ambao mko hapa leo. Mtapimwa kwa kuangalia mafanikio ya walengwa".
Aidha Mkurugenzi Wakili Muhoja amesisitiza kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji katika ngazi ya jamii kwa kuhakikisha watumishi wanafuatilia shughuli za mfuko wa maendeleo ya jamii hasa zile zinazohusu ustawi wa walengwa ili zilete tija.
Kwa Upande wake Muwakilishi wa Mkurugenzi wa TASAF, Bibi Irene Shayo amewashukuru washiriki waliofika kupata mafunzo hayo na kuwataka kuwa makini kwa kipindi chote cha mafunzo ili mwisho wakafanye kazi kwa uadilifu na umakini ili kufikia malengo ya serikali.
Akiwasilisha mada mbalimbali amesisitiza na kutoa ufafanuzi juu ya umuhimu wa warsha za jamii kwa walengwa pamoja na umuhimu wa kuzingatia muda katika ufanyikaji wa warsha hizo ili kufanikisha shughuli hizo kwa wakati
"Ni lazima kuwepo na ratiba maalumu kuhusu warsha za jamii mtakazokuwa mnazifanya hii itasaidia kuwepo kwa mpangilio na kufahamu nini kifanyike kwa wakati gani na kwa kiasi gani". Amesisitiza.
Kadhalika amezungumzia matumizi sahihi ya lugha kwa walengwa kwani inaweza kupelekea kuzuka kwa mtafaruku baina ya Mlengwa na Mratibu kusipokuwepo kwa matumizi mazuri na sahihi ya lugha.
Mnapokwenda katika warsha za jamii mzingatie lugha nzuri na yenye utu ndani yake msiwaite vilema ni watu wenye ulemavu na sio Kipofu ila ni Mtu mwenye uoni hafifu au asiyeona kabisa, Amesisitiza.
Mratibu wa Mpango Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Bibi Agatha Lugome ametoa maelekezo kwa washiriki wa mafunzo kuwa makini na kuzingatia kanuni za mafunzo lakini pia kuwa makini kipindi chote cha mafunzo ili kuleta ufanisi mzuri wakati wa utekelezaji katika vijiji.
Aidha akijibu changamoto mbalimbali zilizoainishwa na washiriki na kuonekana kuwa vikwazo kwenye utekelezaji wa kuwahudumia walengwa wa mpango Bi. Agatha amesema changamoto ni nyingi lakini kubwa ni kutokuzingatiwa kwa muda na kupelekea kuibuka kwa changamoto zingine.
"Tatizo kubwa hapa ni muda na hili linatokana na uhaba wa magari ambayo yamekuwa kikwazo ila ninaahidi kuyafanyia kazi ili kutokujirudia kwa wakati mwingine".
Washiriki pia wamepata nafasi ya kutoa matarajio yao mara baada ya mafunzo na wengi wao wameonesha kufurahishwa na mafunzo haya na kutaja matarajio chanya katika utendaji kazi wao.
Warsha hizi zitafanyika mara moja kila baada ya miezi miwili kulingana na mzunguko wa dirisha la malipo na litafanyika katika vituo vya malipo, walengwa watatakiwa kuhudhuria bila kukosa.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa