DC Kessy Awataka Wananchi Kutofanya Uharibifu wa Mazingira na Kutunza Vyanzo vya Maji na Kupanda Miti Rafiki wa Maji
“Suala la uharibifu wa mazingira nimelitoa kwa uzito wake na kutaka wananchi wazingatie kutunza mazingira na kupanda miti rafiki wa maji. Kauli hii naitoa kwa uchungu mkubwa sana kwani misiti inaharibiwa kwa kukatwa hovyo na kuchomwa mkaa”
Kauli hii imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Veronica Kessy alipokuwa akitoa hotuba fupi katika Mkutano wa Kawaida wa Baraza la Madiwani kwa Robo ya Pili kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023, ambao umefanyika katika Ukumbi wa Siasa ni Kilimo 21/02/2023.
“Sheria iliyowekwa ya kuomba kibali cha kusafisha mashamba inawezekana ikabadilishwa, kwani mtu akiomba kibali cha kusafisha shamba kama alivyoomba badala yake anachoma mkaa, na kupelekea kuharibu mazingira”. Amesema Mheshimiwa Kessy.
Mheshimiwa Kessy ameendelea kusema kuwa, misitu inasaidia sana kuongeza kiwango cha mvua pia kuweka mizinga ya nyuki na kuvuna asali.
Naye Mbunge wa Viti Maalum Mheshimiwa Grace Tendega ambaye amepata nafasi ya kuhudhuria kikao hicho, ameshukuru kwa wajumbe kutoa maoni mbalimbali, naye kama Mbunge ataenda kufanyia kazi kama alivyotumwa. Pia amesisitiza suala zima la mapato, na kusema kuwa bila mapato Halmashauri haiwezi kufanya maendeleo yoyote.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kalenga Mheshimiwa Jackson Kiswaga amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha za miradi ambayo inaendelea kutekelezwa katika Halmashauri.
Mheshimiwa Kiswaga ameongeza kusema kuwa, ataendelea kuomba fedha ziletwe katika Halmashauri ili miradi na maboma ambayo bado hayajamalizwa yaweze kukamilika na kutumika.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri Mheshimiwa Stephen Mhapa amewasisitiza wananchi wanaonufaika na mikopo ya Asilimia 10, ya Makundi ya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu kuwa, mara wanapokopeshwa basi wafanye marejesho kwa wakati ili kutoa nafasi kwa wengine waweze kukopa.
Mheshimiwa Mhapa ameongeza kusema kuwa, kuanzia sasa utafanyika utaratibu wa kuwafuatilia wale wote ambao walikopa muda mrefu na hawajafanya marejesho ili waweze kuwachukulia hatua.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa