Mkutano wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ulifanyika kuanzia tarehe 15-17/08/2022 katika Ukumbi wa Siasa ni Kilimo ambapo kila siku ya mkutano kulikuwa na matukio tofauti.
Siku ya kwanza ya mkutano ilikuwa ni kuwapongeza Walimu wa Shule za Sekondari waliofanya vizuri katika usimamizi wa ujenzi wa madarasa na usimamizi wa taaluma kwa mwaka wa fedha 2021/2022 na kupata ufaulu mzuri Kitaifa na Kimkoa, ambapo vyeti vya pongezi vilitolewa kwa Walimu hao.
Katika Mkutano huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mh. Steven Mhapa aliwaambia walimu hao kuwa, “pamoja na pongezi hizi kuna changamoto mbalimbali zilijitokeza lakini Walimu waliendelea kufanya juhudi katika kuinua taaluma. Pia Mh. Mhapa aliwaeleza walimu ambao shule zao hazikufanya vizuri kitaaluma, kuongeza juhudi katika usimamizi wa wataaluma kwa ujumla”.
Aidha walimu hao walielezwa kuwa, wanatakiwa kutojihusisha na masuala ya siasa kwani jambo hili hushusha taaluma yao na ya wanafunzi.
Shule za Sekondari ambazo zilifanya vizuri katika usimamizi wa ujenzi wa madarasa ni Tanganzozi, Wasa, Nyerere, Pawaga, Mwana, Nyang’oro, Lipuli, Luhota, Lumuli, Makifu, Mgama, William Lukuvi, Mlowa, Furahia. Idodi, Isimila, Ismani, Izazi, Kalenga, Kiwele, Kidamali na Kimaiga.
Shule za Sekondari ambazo zilifanya vizuri katika mitihani ya Kidato cha Nne 2021ni Ifund, Ismani, Idodi, Mtera, Wasa, Kiponzero, Nyerere, Kiwele, Furahia, Ilambilole,Mwana, Mgama, na Lyasa.
Pia shule za Serikali ambazo zilizofanya vizuri kwa asilimia mia ni Lipuli na Furahia. Kadhalika shule Binafsi zilizofanya vizuri kwa asilimia mia moja ni St. John Paul, St. Marys, St. Thomas Nyabula, God of Life, St. Dominic Savion a St. Theresa.
Aidha kulilikuwa na shule Tano Bora Kimkoa zimefanya vizuri; St. Marys Ulete, St. John Paul, St. Dominic, St. Theresa na Shule ya Ufundi Ifunda.
Pamoja na kutoa pongezi kwa Walimu wa Sekondari waliofanya vizuri pia Mh. Mhapa aliwaomba Waheshimiwa Madiwani kutoa taarifa za Kata zao na kuanisha changamoto na mafanikio.
Siku ya Pili ya Mkutano Mh. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mh. Steven Mhapa baada ya ufunguzi wa kikao, alitoa salamu za mapokezi ya Mh. Rais Samia Suluhu Hassan, na kueleza kutoa changamoto za kila Kata, ambapo changamoto mbalimbali zilianishwa ikiwamo jinsi ya kuinua mapato ya Halmashauri. Wajumbe walieleza namna ya kubuni vyanza vipya vya mapato na kuboresha vile vilivyopo. Vyanzo vipya ni kama nyumba za kupangisha, kumbi za sherehe na starehe, vyoo vya kulipia, standa katika maeneo ya Ihemi Kata ya Mgama na Itunundu, ujenzi wa mageti madogo katika maeneo ambayo malighafi zinatoko mfano Kata ya Kiwele.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mh. Mohamed Moyo alipata nafasi ya kuzungumza na akasema kuwa, “kunatakiwa kuwe na usimamizi wa fedha za mikopo baada ya marejesho, kwani Waheshimiwa Madiwani wanatakiwa wajue fedha hizo zinatumikaji baada ya kurejeshwa”
Ameongeza kusema kuwa, migogoro ya ardhi katika Kata inatakiwa itatuliwe haraka kwa kuwaita wapimaji ili wapime na kila mmiliki apate hati miliki, kwani njia mojawapo ya kutatua migogoro.
Aidha Mh. Moyo amewata wajumbe waoneshe ushirikiano katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru ambapo kila sehemu utakapopita, na si kwenye maeneo yao tu, kwani ni suala muhimu katika maendeleo.
Pia Mh. Moyo amewashukuru wajumbe na watendaji wote kwa mapokezi mazuri ya kumpokea Mh. Rais Samia Suluhu Hassan, kwani imetupa heshima kubwa sana kwa Wanairinga.
Katika Siku ya Tatu ya Mkutano, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mh. Steven Mhapa, alisema namna ya kufanya uchaguzi wa kumchagua Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, ambapo zoezi hufanyika kila mwaka. Pia kuteua Kamati za Kudumu za Baraza la Madiwani. Katika uchaguzi huo wa Makamu Mwenyekiti, Mh. Mathew Marcus Nganyagwa alipata kuwa mshindi na kuchukua nafasi ya hiyo ya Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri.
Wakati huo huo kulikuwa na zoezi la utoaji wa vyeti vya pongezi kwa viongozi waliohudumu katika Kamati za Kudumu na wamemaliza muda wao. Pia pongezi na vyeti vilitolewa kwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri aliyemaliza muda wake, na pongezi kwa Makamu Mwenyekiti mpya aliyechaguliwa.
Naye Afisa Mipango wa Halmashuri ya Wilaya ya Iringa Bwana Wapa Mpwehwe akitoa taaria ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri amesema, katika zoezi la ukusanyaji wa mapato limefikia asilimia 87, na kwamba ili kuendelea kuboresha ukusanyaji wa mapato wanatakiwa kutumia njia ya kielektroniki ili kuzuia mapato yasipotee.
Katika kuchangia jinsi ya kuboresha miradi ya maendeleo Halmashauri wajumbe walisema kuwa, inatakiwa kuongeza mifereji ya umwagiliaji katika maeneo mbalimbali ya kilimo na si kutegemea mvua pekee. Pia Madiwani wanatakiwa kuwasisitiza wananchi kuchangia nguvu kazi katika kazi za maendeleo, hii itasaidia kukamilisha miradi kwa wakati na kuwasaidia wananchi kuanza kutumia miradi hiyo mara moja.
Mwisho Mwenyekiti wa Halmashauri aliwataka Madiwani kuwahizimiza wananchi kujitokeza katika Sensa ya Watu na Makazi siku ya tarehe 23/08/2022.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa