Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Kheri James ameongea na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya katika ukumbi wa makao makuu ya Halmashauri uliopo katika kijiji cha Ihemi Machi 15, 2024 ambapo amewataka watumishi kufanya kazi kwa kuzingatia umoja na uwajibikaji.
“Watu wakishakuwa wamoja maana yake watawaza pamoja na kupanga pamoja kisha kuwajibika kwenye elimu, utumishi, uhandisi, ustawi wa jamii, maendeleo ya jamii, sharia na kila mmoja atimize wajibu wake”
Aidha, Mhe. Kheri ametaja vipaombele vya kuzingatiwa katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ambavyo ni; Ukusanyaji wa mapato, utekelezaji wa miradi ikisimamiwa vema na kukamilika, ulinzi na usalama, utatuzi wa kero za wananchi na utekelezaji wa maagiza ya ngazi za juu.
Sanjari na hayo Mhe. Kheri amebainisha vyanzo vya migogoro na kero nyingi za wananchi hasa kwenye upande wa ardhi kwa sehemu kubwa ni kutokuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi ambapo amewaasa maafisa ardhi kupitia ofisi ya Mkurugenzi mtendaji (W) kupanga maeneo na kuyapima ili kila mtu apate haki ya eneo lake na kwa wakati.
Mhe. Kheri James amekuja na kauli mbiu ambayo inapaswa kuzingatiwa na watu wote kwenye utekelezaji wa majukumu mbalimbali ambayo ni “Iringa Imara, Tutaijenga kwa Umoja na Uwajibikaji”
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Bi Saumu Kweka amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa nasaha zake ambazo ni kama semina elekezi na kuahidi kwamba yote yaliyotolewa yatapelekwa kwenye utekelezaji.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa