Madiwani walia na Upungufu wa Watumishi Iringa – DC
Ummi Mohamed (Afisa Habari na Uhusiano, Iringa-DC)
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Iringa limefanya Mkutano wa siku mbili kuanzia tarehe 8 na 9 mwezi Februari, mwaka huu 2022 kupitia na kujadili taarifa kutoka katika kamati mbalimbali za kudumu za Halmashauri hiyo.
Akiongoza Mkutano huo wa siku mbili Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mh. Stephen Mhapa aliwataka Waheshimiwa madiwani kujadili na kuhoji kwa hekima kwa kuwa lengo la Mkutano huo ni kwa ajili ya ustawina maendeleo ya Wananchi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.
“Taarifa hizi ni kwa ajili ya wananchi wetu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, ambao wametutuma tuwawakilishe hivyo nawaomba tujadili kwa hekima ili wananchi wetu wapate mahitaji na huduma kutoka kila Idara ya Halmashauri hii ambayo ipo ndani ya uwezo wetu”alisema.
Aidha katika Mkutano huo Waheshiwa Madiwani walijadili masuala mbalimbali likiwemo la upungufu wa watumishi katika Halmashauri hususani katika Idara ya Utawala, Afya,Elimu msingi na sekondari, na kuomba suala la watumishi wa Idara ya Utawala lifanyiwe kazi na kupewa kipaumbele maalum kwa kuwa miradi mingi inayoenda katika Kata na Vijiji inasimamiwa na Watendaji hivyo uwepo wao ni muhimu sana.
Pamoja na kujadili taarifa za kamati za kudumu Waheshimiwa Madiwani walipata fursa ya kujadili rasimu ya mpango wa bajeti kutoka kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Barnaba Selemeni Jabir amesema Ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2022/2023 inatarajia kutumia kiasi cha bilioni ……………
Lakini pia, walipitia mpango wa bajeti kutoka kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA ) Mhandisi Masoud Samila amesema kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ofisi yake inatarajia kutumia kiasi cha Billion 7.138 katika kutekeleza shughuli za miradi ya Maji na Usafi wa Mazingira katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.
Wakati huo huo,Afisa Ardhi na Maliasili Bw.Geofrey Kalua alitoa elimu kwa Baraza la Madiwani, Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi – CCM na Serikali waliohudhuria Mkutano huo ambapo alieleza dhamira ya Serikali ya awamu ya sita ya kutaka kuboresha anwani za makazi ili kurahisi mawasiliano.
Bw. Kalua alieleza namna ya kupata anwani ya makazi kwa kutumia simu ambapo alisema ili uweze kupata huduma ya anwani ya makazi (Post Code) unatakiwa Kubofya alama ya *152# kisha unachagua 3 kisha 2 kisha 1 kisha utachagua namba ambayo ina herufi ya kwanza ya mkoa wako kisha utapata orodha ya mikoa utachagua namba ya Mkoa wako na kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ipo namba 1 baada ya kuchagua Mkoa.
“Waheshiwa Madiwani tunaomba ushirikiano wenu wa hali na mali pindi zoezi hili litakapoanza kwa kuwajulisha wananchi na Viongozi wa Vijiji na Vitongoji watupokee katika maeneo yao na kutupa Ushirikiani ili kulifanikisha zoezi hili kama lilivyopangwa kutekelezwa na Serikali”alisema Bw.Kalua.
Hata hivyo Baraza hilo pamoja na Wageni waalikwa Viongozi wa Chama na Serikali walipewa elimu ya ukaguzi wa ununuzi na mapokezi ya dawa katika Zahanati,Vituo vya Afya na Hospitali ya Wilaya kutoka kwa Mganga Mfawidhi wa Wilaya Dkt.Samwel Marwa elimu ambayo itawasaidia Waheshimiwa madiwani na viongozi kuweza kuhakiki kama hakuna ubadhirifu unaoweza kutendeka na baadhi ya watumishi ambao sio waaminifu.
“Naomba pamoja na elimu hii ya ukaguzi isiende kuingilia utendaji wa kitaalam kwa kuwa wahusika ambao wanatoa huduma za utabibu wanafahamu dawa gani inatibu ugonjwa gani hivyo tunaweza kufanya ukaguzi lakini naomba kutoa rai ya kutoingilia masuala ya kitaaluma” alisema Dkt.Marwa.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa