Mhe. Mhapa Asisitiza Mahusiano na Mawasiliano Mazuri baina ya Wahe. Madiwani na Wataalamu kutoka Halmashauri
Na Ofisi ya Habari na Uhusiano,Iringa-DC
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mhe. Stephen Mhapa ameongoza Mkutano wa Baraza la Madiwani Robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2021/2022 katika ukumbi wa Halmashauri siasa ni kilimo 10/05/2022.
Akitoa taarifa Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Mhapa amewashukuru Wah. Madiwani kwa kuendeleza ziara za kikazi na amethibitisha Baraza kupokea taarifa za utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kimaendeleo za kata kwa robo ya tatu Machi hadi Mei 2021/2022.
Katika kuwasilisha taarifa hizo za maendeleo ya kata Waheshimiwa Madiwani kutoka Kata mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwa kiasi kikubwa wameshukuru Serikali kwa kuwaletea fedha za maendeleo lakini pia wamemshukuru Mwenyekiti, Mkurugenzi na Wataalamu kutoka Halmashauri kwa ushirikiano wanaouendeleza ili kufanikisha shughuli za maendeleo kwa kila Kata.
Waheshimiwa Madiwani kutoka Kata mbalimbali wamewasilisha taarifa zao kwa mtindo wa kusoma changamoto ili kuwafanya wataalamu kuwa na uelewa ni wapi pa kuanzia, kuongeza nguvu na kutafuta njia mbadala katika kutatua changamoto hizo.
Miongoni mwa changamoto zilizowasilishwa kutoka Kata mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ni pamoja na Suala la ubovu wa bararabara kutokana na mvua zilizonyesha zimekuwa na athari kali, ukosefu wa maji ambayo kiujumla inaathiri shughuli za kimaendeleo
Upungufu wa maji, ukosefu wa hosteli, upungufu wa matundu ya vyoo, uchakavu wa vyoo, ukosefu wa nyumba za walimu na wataalam wa afya, ukosefu wa walimu wa kike, upungufu wa watendaji wa Vijiji, Ukosefu wa usafiri kwa wataalamu n.k
Wakiwasilisha changamoto hizo Wah. Madiwani wameiomba Halmashauri iweze kusaidia na kutia nguvu maeneo hayo yenye changamoto ili kupunguza kama sio kumaliza kabisa matatizo hayo ambayo yameonekana kuwa kikwazo cha maendeleo ya Kata na Halmashauri kiujumla.
Akitoa msisitizo kwa yaliyowasilishwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mhe. Mhapa amesema; kwa ujumla wake tumeona bado tuna tatizo kubwa la umeme katika vitongoji vyetu tujue ni vingapi havina umeme na hii itatusaidia katika utoaji wa taarifa katika vikao mbalimbali ikiwemo kikao cha wilaya
Lakini pia amesema tuna tatizo kubwa la umaliziaji wa majengo mbalimbali ya zahanati, nyumba za walimu, madarasa, mabweni ninaomba hilo lote liwekwe sawasawa, wananchi wamejitihadi kwa nafasi zao hivyo serikali lazima itambue,
"Na ikiwezekana majengo yote yapigwe picha kwa ajili ya kumbukumbu na ipelekwe serikalini ili na wao pia watusaidie tulipoishia".
Watendaji wa vijiji nao ni changamoto kubwa na shughli za maendeleo zinahitaji watendaji wa Vijiji ili waweze kuhamasisha na kusimamia shughuli hizi za kimaendeleo, tunatakiwa tujue ni namna gani tunapata hawa watendaji, lazima tuchukue hatua za ziada. Amesisitiza.
Pia Mwenyekiti Mhe. Mhapa amewaagiza Wakuu wa Idara kufuatilia na kuleta majibu juu ya hoja na changamoto zote zilizowasilishwa na kuwataka Waheshimiwa Madiwani kusimamia fedha za serikali zinazoletwa, kuhakikisha shughuli zinafanyika na kujitahidi kusemea.
Akifunga Mkutano wa Baraza la wah. Madiwani kwa siku ya kwanza Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mhe. Mhapa ametoa shukrani kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Bashir Muhoja na wataalamu wa Halmashauri.
"Niwashukuru sana Mkurugenzi na wataalamu, tumeshuhudia madiwani takribani wote wamewashukuru sana na mimi naungana nao kuwapongeza, niwatake wataalamu kuwa na mawasiliano mazuri na madiwani ili kuleta ufanisi katika shughili za kimaendeleo.
Mkutano wa Baraza la Wah. Madiwani linatarajiwa kukutana tena kwa siku ya pili tarehe 11/05/2022 kwa ajili ya maswali ya papo kwa papo na kupokea taarifa mbalimbali za Kamati za Kudumu za Halmashauri.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa