NEMC, WAMILIKI WA KUMBI ZA STAREHE WAKUTANA NA RC
Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Dendego amesema “kumekuwa na malalamiko mengi katika jamii zetu, malalamiko ya wagonjwa hawalali hata sisi wenyewe kawaida hatulali lakini pia upande wa pili kuna wenzetu wamewekeza na wanahitaji kupata kile walichowekeza kutokana na uwekezaji huo kwa hiyo kwa kutambua hilo Serikali imetutaka tukae pamoja lengo ni kujenga na sio kubomoa”.
Mhe. Dendego ametaka mazungumzo yafanyike kwa kuzingatia maslahi ya pande zote ili wafanya biashara wafanye kazi zao na wanufaike na uwekezaji wao, vilevile jamii nayo isipate usumbufu kutokana na kelele zinazozalishwa.
Kwa upande wa Mipango Miji Mhe. Dendego amesema, “Mpaka tumefika hapa lazima tujitathmini, tuna tatizo sana kwenye suala zima la Mipango Miji katika Miji yetu, ambayo haijapangiliwa kulingana na mahitaji yetu. Katikati ya makazi kuna nyumba za Ibada, masoko, nyumba za starehe, magenge nk. Hii sio sahihi”. Amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kulifanyia kazi suala hili la Mipango Miji hasa kwa maeneo ambayo bado hayajasongamana.
Naye Mtaalamu kutoka NEMC ametoa wasilisho lake la masuala ya mazingira amesema, “kuna viwango vya kelele ambavyo havitakiwi kwenye maeneo mbalimbali mfano eneo la makazi, viwanda, maeneo ya starehe n.k hivyo wamiliki wa kumbi za starehe na baa mnatakiwa kuwa na vifaa vya kupima viwango vya kelele ili kutovuka kiwango elekezi kutokana na eneo”.
Kwa upande wao wamiliki wa kumbi za starehe wamekubaliana na wasilisho lililotolewa na kuomba kuwa elimu hii iwe endelevu ili kuwafikia wadau wengi zaidi yaani washereheshaji, wamiliki wa kumbi na waongoza mziki (DJ), ili kuwa na uelewa wa pamoja na kurahisisha utekelezaji wake jambo ambalo limekubaliwa na kupokelewa.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa