NFRA Yaokoa Baa la Njaa kwa Bei Nafuu
Wakala wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula (NFRA) waokoa jamii kutoka kwenye janga la njaa kwa kuwauzia wananchi waliothirika na baa hilo kwa bei nafuu.
Kikao kifupi kimeketi na Mwenyekiti wa Halmashauri kwa Kushirikiana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Ndugu Isdory Karia, baadhi ya Waheshimiwa Madiwani na baadhi ya Watendaji wa Kata husika, ambao wameathirika sana na baa hili, ili kujua namna gani chakula hiki kitawafikia walengwa.
Mhasibu wa Kanda ya Makambako Ndugu Steven Lyapa amesema, “tutasambaza mahindi ya chakula kila Kata yenye uhitaji, na kwamba kila Kata kutakuwa na sehemu maalumu ya kuhifadhia mahindi hayo. Hivyo tunahitaji ulinzi na usalama wa chakula hicho na wale wanakuja kusambaza, na kuwahamasisha wananchi waje kununua mahindi haya kwa bei nafuu ya Shilingi 780/= kwa kilo moja”
“Chakula hiki ni mali ya Serikali, hivyo hatutegemei akatokea mtu baki ambaye siyo muhitaji akaja kudhulumu haki ya wanufaika. Ninyi mnafahamu idadi ya Kaya katika maeneo yenu”. Amesema Ndugu Lyapa.
Naye Afisa Ugavi wa Kanda hiyo Ndugu Emmanuel B. Nyanda amesema kuwa, “Kila mnunuzi atakayekuja kununua lazima apimiwe kiasi halisi anachohitaji, kwani kila kituo cha mauzo kutakuwa na mzani kwa ajili ya kupima ambao umehakikiwa na Serikali. Japo kila mfuko una ujazo wa Kilogram 50, lakini ni muhimu ukapimwa tena wakati wa uuzaji kwa ajili ya uhakiki zaidi” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri Mheshimiwa Stephen Mhapa, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusikia kilio hiki cha baa la njaa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, na kufanya Wakala wa Chakula wa Taifa kushughulika na jambo hili kwa haraka sana.
NFRA wataanza kutoa chakula tarehe 25/02/2023 kwa Kata Tano awamu ya kwanza ambazo ni Kata za Malengamakali Tani 30, Migoli Tani 30, ikifuatiwa na Izazi Tani 20, Nzihi Tani 30 na Mlowa Kata 20 na kufanya jumla ya Tani 130 kutolewa. Kwa awamu nyingine watatoa kwa Kata za Kihorogota na Kiwere ambako pia kuna uhitaji mkubwa wa chakula.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa