Halmashauri ya Wilaya ya Iringa yaishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kukarabati shule Kongwe.
Na Ummi Mohamed (Afisa Habari na Uhusiano,Iringa- DC)
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Bw. Wapa Mpwehwe amesema Serikali ya awamu ya tano imetoa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 1.4 kwa ajili ya kukarabati majengo ya shule kongwe za sekondari Tosamaganga na Ifunda wasichana kwa mwaka wa fedha 2019 /2020 na ukarabati huo unaendelea.
Akitoa ufafanuzi Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Bw.Mpwehwe amesema serikali imetoa milioni 650 kwa ajili ya ukarabati shule ya Sekondari ya Tosamagana na milioni 767 kwa ajili ya shule ya Sekondari ya Ifunda wasichana.
“Ukarabati katika shule hizi mbili unafanywa na serikali bila kuhusisha nguvu ya wananchi na kama ambavyo mmeona kazi iliyofanyika na inayoendelea kufanyika katika ukarabati huu”amesema Bw. Mpwehwe.
Kwa upande wake Mwnyekiti wa kamati ya Elimu,Afya na Maji Mh Bruno Kindole alisema;
“Naipongeza sana Serikali kwa kutenga fedha hizi kwa ajili kukarabati miundombinu ya shule hizi kongwe na kuzifanya ziwe na mandhari zinazovutia kujifunza, lakini nampongeza sana Mkurugenzi Mtendaji Bw.Robert Masunya kwa kushirikiana na Wataalam wake wanafanya kazi nzuri sana katika Halmashauri yetu hasa katika miradi ya maendeleo”alisema.
Aidha, Mh.Kindole alitembelea pia,mradi wa kituo cha Afya cha kimkakati kinachojengwa katika Kata ya Ifunda kijiji cha kibena na kujionea mradi wa kituo cha afya ulioanzishwa kwa nguvu ya wananchi.
“Binafsi nimefurahishwa sana na jinsi mlivyojitoa katika suala la maendeleo kwa kujenga hili boma kwa kweli mnastahili sana kupongezwa”alisema na kuongeza;
“Serikali hailali inaona na inafanya kazi sana, iwapo wananchi wanaibua na kuanzisha miradi ya maendeleo katika maeneo yao Serikali haisiti kuweka nguvu ikibaini wananchi kweli wanauhitaji wa huduma wanayoianzisha na ndio maana kiasi hiki cha milioni 200 kimeletwa hapa katika kijiji cha Kibena baada ya kuibua mradi huu wa kituo cha Afya”alisema.
Mh Kindole amesema uongozi wa Kijiji hiko uwe mfano wa kuigwa na vijiji vingine katika shughuli za maendeleo na ameipongeza serikali ya kijiji cha Kibena kwa kuonyesha Ari ya kupenda maendeleo hasa kwa jinsi walivyojitoa katika kuanzisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kimkakati.
Wakati huo huo,Diwani wa Kata hiyo Mh.Elikus Ngweta ameitoa hofu Kamati hiyo na amewahakikishia wajumbe kuwa wananchi hao wanapenda maendeleo na wamedhamilia kukiletea kijiji chao maendeleo hivyo watajitoa kila watakapo takiwa kufanya hivyo.
“Utendaji wa ushirikishaji wa jamii umepelekea wananchi kuwa waelewa na hasa kijiji hiki sio wavivu kabisa tena ujenzi ukikamilika kituo hiki cha afya kiitwe Kibena kwa kuwa wananchi wa kijiji hiki tu ndio wamejitoa katika kata nzima yenye vijiji sita”alisema Mh Ngweta.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa