Atoa wito kwa taasisi mbalimbali za serikali kuendeleza zoezi hili, ahimiza miti ya matunda ipandwe mashuleni ili kusaidia kwenye suala la lishe
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Kheri James amezindua rasmi kampeni ya upandaji wa miti katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa. Uzinduzi huo umefanyika katika ofisi za makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Iringa yaliyopo Ihemi Januari 29, 2026.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa kampeni hiyo Mhe. Kheri James ametoa wito kwa taasisi mbalimbali za serikali kuendelea na zoezi la upandaji wa miti kwa madhumuni ya kimkakati kulingana na mazingira ya taasisi husika ambapo ametoa siku 14 kutekelezwa kwa zoezi hili.
Aidha kwa upande wa taasisi za elimu hasa shule za msingi na sekondari, miti ya matunda ipandwe ili kusaidia uboreshaji wa lishe na utamaduni huu uanzie mashuleni na baadaye majumbani.
“Leo nachukua fursa hii kuwahamashisha wananchi wa Mkoa wa Iringa kwamba kampeni yetu ya upandaji wa miti imeanza rasmi hapa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Iringa katika eneo hili la Ihemi, matarajio yetu ni kuona kata zote, tarafa zote, vijiji vyote viongozi mnakwenda kuhamasisha zoezi la upandaji miti kwa maelekezo mahususi”. amesema Mhe. Kheri.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Ndg. Robert Masunya amesema, maagizo ya Mkuu wa Mkoa yamepokelewa na atahakikisha kuwa miti itapandwa hasa katika taasisi mbalimbali ikiwemo shule za msingi na sekondari na kuhakikisha kuwa miti hiyo inatunzwa.
“Kazi yangu mojawapo ni kusimamia miti yote ipelekwe kwenye taasisi kwa sababu tunavyo vitalu hapa na tumeshaotesha miti, kuhakikisha inagawiwa lakini kubwa ni kuhakikisha miti yote iliyopandwa inakuwa na kutunzwa” amesema Ndg. Masunya
maadhimisho ya mwaka huu yamepambwa na kauli mbiu isemayo; “Misitu ni Uchumi Endelevu, Tuihifadhi kwa Maendeleo ya Taifa”.


Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa