Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe.Halima Dendego ametoa agizo kuwa wanafunzi wote wawe wameripoti shuleni ifikapo Januari 30, 2024. Ameyasema hayo akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu tarafa ya Pawaga katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ambapo 17.01.2024 ametembelea shule ya Sekondari Mlenge, shule ya Msingi Mseke, kufanya mazungumzo na viongozi wa vijiji na baadaye kufanya mkutano wa hadhara katika kijiji cha Itunundu kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
“Tumeona elimu ya msingi na sekondari shule zimejengwa zinang’aa kabisa lakini nimepita watoto hawapo shuleni kwa hiyo kazi ninayowapa ninyi wananchi pamoja na watendaji kila mmoja ahakikishe kwa siku chache hizi zilizobaki kuelekea tarehe 30 Januari kila mtu mtoto wake yupo shuleni, kama ni awali, msingi au sekondari awe darasani. Kwa hiyo kupitia kikao hiki naagiza hayo nasheria ziko wazi, asiyepeleka mtoto wake shule ni miezi sita jela na faini au kifungo bila faini”.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Wakili Bashir Muhoja amesema miundombinu yote inayohitajika ipo tayari kwa ajili ya kupokea wanafunzi na kwamba maeneo mengine ambayo bado yanachangamoto hasa kwa upande wa matundu ya vyoo yatafanyiwa kazi na hatua kadhaa zimeshaanzakuchukuliwa.
Kwa upande wa miundombinu ya maji Mhe. Dendego amesema amejionea hali ya maji kwamba yapo ya kutosha lakini sio masafi hivyo ameahidi kuwa ndani ya wiki mbili suala hilo litatafutiwa suluhu kwa kushirikiana na meneja wa RUWASA.
Aidha Mhe. Dendego amepata wasaa wa kusikiliza kero na changamoto za wananchi ambapo kwa sehemu kubwa ni migogoro ya ardhi na kuipatia suluhu. Pia amewaasa wananchi kutokuuza ardhi kwani tayari kulishawekwa zuio na anayetaka kuuza mashamba apate kibali cha serikali ili serikali ya kijiji ijiridhishe kuhusu eneo hilo. Na kwa maeneo ya serikali yaliyouzwa bila kufuata utaratibu, Mhe. Mkuu wa mkoa ametangaza kufuta mauziano hayo hadi hapo taratibu zote za mauziano zitakapofuatwa kama mauziano yatahitajika.
Ziara hii ya Mkuu wa mkoa wa Iringa katika tarafa ya Pawaga inaendelea kwa siku ya tatu ikiwa na lengo la kutatua kero na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamojana changamoto za ardhi.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa