RC Serukamba Awaonya Watumishi kwa Kutofanya Kazi kwa Uadilifu
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Peter Serukamba amewaonya Watumishi ambao hawafanyi kazi kwa uadilifu na kuendana na kasi ya Mheshimiwa Rais katika kutekeleza majukumu ya kazi zao.
Mhe. Serukamba ameyasema hayo alipokuwa katika ziara yake Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Septemba 23, 2024 akikagua maendeleo ya miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo.
“Mkurugenzi tafuta mtu wa manununuzi mwingine ambaye anaweza kusaidia kufanya kazi kwa haraka katika mifumo yenu, pia Wakandarasi wote ambao wanachelewesha kuleta vifaa katika maeneo ya ujenzi waondoeni na kuleta wengine ambao wataendana na kasi tunayotaka sisi kwani miradi hii imechelewa sana kuanza” amesema.
Mhe. Serukamba ameendelea kusema kuwa, “Kila mtu atimize wajibu wake, kwani hakuna mtumishi aliyepangwa katika Halmashauri hii kwa bahati mbaya. Wabunge wenu wanatafuta fedha kwa bidii kubwa ili kuleta kwa wananchi kufanya maendeleo mbalimbali, lakini nyie mnamuangusha sana Mhe. Rais. Haifai kukumbushana kila kitu”.
Baadhi ya miradi aliyotembelea katika ziara hiyo ni Kituo cha Afya Isimani katika jengo la mapokezi ya wagonjwa wa nje, Shule ya Sekondari Isimani mradi wa Mabweni, Kata ya Kihorogota, Zahanati ya Ikengeza Kata ya Kising’a, Shule ya Sekondari Mboliboli Kata ya Mboliboli, ujenzi wa sekondari mpya Kijiji cha Kimande Kata ya Itunundu, ujenzi wa madarasa mawili katika Shule ya msingi Mkombilenga Kata ya Ilolompya, ujenzi wa madarasa 2 na bweni shule ya sekondari William Lukuvi Kata ya Ilolompya.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Kheri James amesema, atafanya ziara yake kijiji kwa kijiji ili aongee na Vijana wa kila eneo kwa ajili ya kuhamasisha maendeleo ya eneo husika. Pia amewataka wananchi kujitolea katika miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa