TCRA Yawakumbusha Wanahabari Kufuata STK za Kazi Zao
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ni Taasisi ya Serikali yenye kusimamia Sekta ya Mawasiliano nchini.
Mamlaka hiyo imekutana na Wanahabari wa Mkoa wa Iringa Mei 03, 2024 katika Ukumbi wa Maktaba ya Mkoa wa Iringa na kukumbushana masuala muhimu ya kuzingatia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, kwani Mamlaka ina jukumu la kusimamia Sekta hii katika nyanja mbalimbali, na kuhakikisha kuwa Sekta ya Mawasiliano inafanya vizuri.
Akitoa maelezo ya namna Mamlaka hiyo inavyofanya kazi wakati akifungu kikao kilichowakutanisha Wanahabari hao Meneja wa Kanda Nyanda za Juu Kusini Mhandisi Boniphace Shoo amesema, “Wanahabari ni muhimu kufanya majukumu yenu kwa kufuata mambo matatu muhimu, ambayo ni Sheria, Taratibu na Kanuni (STK) ili kusiwepo na vikwazo kutoka Mamlaka hiyo na jamii kwa ujumla”.
Mhandisi Shoo ameendelea kusema, “kwa mfano Mtangazaji ni muhimu kutumia lugha ya staha, kumlinda mpokeaji huduma, kuelimisha jamii, kuburudisha, hii yote itafanya Sekta hii kushamili na kutokuwepo na malalamiko yoyote, na kwamba sisi kama Mamlaka tumepewa jukumu la kuhakikisha tunafuatilia hatua kwa hatua ili kuhakikisha hakuna ukiukwaji wa maadili”.
Akitoa mada ya Pili inayohusu Leseni Mhandisi Sunday Richard kutoka Makao Makuu ya Mamlaka amesema, “Mtoa huduma lazima azingatie anafanya kazi yake kwa kufuata leseni yake aliyoomba, kama mtu ameomba leseni ya kusambaza vifaa vya mawasiliano basi asichanganye na kazi nyingine. Kama mtoa huduma anahitaji kuongeza au kupanua huduma yake basi atalazimika kuomba kubadilishiwa leseni yake inayoendana na huduma anayotaka kutoa.”
Mhandisi Sunday amesema pia, kuna aina nyingi za leseni kulingana na huduma mtu anayotaka kutoa, kwani kuna Leseni Kubwa, Leseni Ndogo, Leseni za Makundi ya mitandao. Pia amesema namna ya kuomba leseni katika mifumo ya Mamlaka na viambatishi vinavyotakiwa kuwepo wakati mtoa huduma anaomba leseni.
Naye Mhandisi Balongo Mwesiga Kutoka Makao Makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ameongelea Kitengo cha Ufuatiliaji na Utekelezaji na kusema namna kitengo hicho kinavyofanya kazi, ikiwa ni pamoja na kusimamia michakato ya utekelezaji na uzingatiaji wa shughuli za Sekta 3 ambazo ni Mawasiliano/Intaneti, Utangazaji na Posta. Pia kuandaa, kupitia na kutekeleza Kanuni, Sheria na miongozo, na ufuatiliaji wa utekelezaji wa majukumu kwa ujumla.
Mada ya Nne ambayo ilitolea na Mhandisi Kisaka kutoka Makao Makuu ya Mamlaka, inayohusu Kanuni za Radio na Runinga ambayo ilitolewa mwaka 2008 na kufanyiwa maboresho 2022, amesema mtangazaji anapaswa kuzingatia haki za watoto, kutotoa maoni binafsi, kutoweka tangazo la biashara katika kipindi maalumu kama Bunge na mengine mengi.
Naye Mhandisi Bathlomeo Titus amesisitiza kupata leseni za maudhui ya kimtandao (Digital), na kufuata kanuni za kutuma maudhui mtandaoni (Parental Guarding – PG).
Baadhi ya Wanahabari walipata nafasi ya kutoa maoni mbalimbali na kuuliza maswali ambapo Wahandisi hao wa Mamlaka ya Mawasiliano waliweza kujibu na kuchukua maoni ili wakayafanyie kazi.
Mhandisi Shoo aliweza kuwashukuru Wanahabari hao na kuendelea kuwasisitiza kufuata STK ili kuepuka kufanya mambo kinyume na maadili.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa