TASAF Iringa DC Wahitimisha zoezi la Ugawaji Vifaa vya Usafi kwa Watoto
Na Ofisi ya Habari na Uhusiano Iringa DC
Shughuli ya ugawaji vifaa vya usafi kwa watoto wa kike wanufaika na mpango wa kunusuru kaya Maskini TASAF Halmashauri ya Wilaya ya Iringa umehitimishwa leo mei 07.
Kwa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa mabox 1738 ya vifaa vya watoto wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini yamepokelewa na kuwapatia watoto 3476 wa wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini.
Vifaa hivi vimegawiwa katika vijiji 82 kwa watoto wa kike kwa majina yaliyotolewa 3476 ikiwa watoto 1641 ni wa sekondari na watoto 1835 ni wa shule ya Msingi.
Akizungumza katika shughuli hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Wakili Bashir Muhoja ambae pia amekuwa mgeni rasmi, amemshukuru Mkurugenzi wa TASAF pamoja na timu nzima kwa uratibu wa zoezi hilo.
Amesema lengo kuu la kutoa vifaa hivyo ni kuhakikisha kuwa mahitaji ya watoto walioko shuleni wanahudhuria masomo vizuri bila kisingizio kutokana na sababu za kibaolojia (Maumbile).
Ameongeza kwa kusema lengo ni kuwafikia watoto walioko mashuleni lakini pia kuna watoto wengine ambao kwa njia moja ama nyingine hawapo mashuleni lakini wana uhitaji,
"Hii ni kama mbegu tunatakiwa tutoe elimu kwa kule ambako mkono wa serikali haujafika basi wadau wajitokeze au jamii yenyewe isimame na ione inawasaidiaje watoto hao". Ameongeza.
Kwa upande wa changamoto Mkurugenzi Mtendaji amesema wamekukumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo kutokuwakuta watoto katika vituo vya ugawaji, baadhi ya wazazi kuja kuwachukulia vifaa hivyo watoto wao nk.
Aidha tumepokea taarifa za kuwa kuna baadhi ya wanafunzi hawana mahitaji muhimu ya shule kama vile sare za shule, Jamani tuendelee kuhamasishana wazazi tuendelee kujibana na tuone umuhimu wa kuwahudumia watoto wetu wapate mahitaji yao ya kielimu. Ameongeza
Kwa upande wa Diwani wa Kata ya Kalenga Mhe. Shakira Kiwanga ambapo shughuli hii imefanyika amemshukuru Mkurugenzi na timu nzima ya TASAF Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwa kufanikisha shughuli hii katika kata ya Kalenga.
Asema kata ya Kalenga wamebahatika kupata vijiji viwili, kijiji cha Isakalilo kwa kuwapatia watoto 15 na kijiji cha Kalenga watoto 50 na kufanya jumla kuwa na watoto 65.
Pia ameishukuru Serikali inayoongozwa na Mhe. Mama Samia Suluhu kwa kuwajali wananchi wake kupitia mpango huu wa kunusuru kaya Maskini TASAF kwa kuzikumbuka kaya hizi maskini na kuzipatia msaada.
"TASAF inawasaidia sana wananchi wetu japo uhitaji wake huwa ni mkubwa sana, huwa tunawaambia kwamba inaenda awamu kwa awamu, wahitaji bado ni wengi sana hivyo tunawaomba waendelee kuziunga mkono kaya hizi".
Ameongeza kwa kusema kuwa kuna haja ya kuongea na wazazi kuhusu matumizi sahihi ya taulo hizo za kike ambazo zimetengenezwa kwa kufuliwa na kuanikwa hivyo wazazi watapaswa kupewa elimu ya kutosha juu ya maandalizi na matumizi ya taulo hizi.
Aidha Kaimu Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Khamis Juma Sabuni amesema kuwa vifaa vilivyotolewa ni pamoja na Sabuni miche miwili, nusu dazani za nguo za ndani, taulo za kike sita zikiwa ni taulo za kufuliwa, mfuko wa kutunzia vifaa na ndoo kwa ajili ya usafi.
Pia amewasisitiza wanufaika kuwa fedha ya masharti matumizi yake ni kama hivyo, yani kuhakikisha watoto wanapata mahitaji yao ya msingi kupitia fedha hizo za masharti
"Na huu ni kama mfano TASAF wameamua kufanya hivi kwa lengo la kuwakumbusha wanufaika kuwa matumizi mengine ya fedha za masharti ni kufanya kama hivi".
Miongoni mwa wanafunzi walionufaika na vifaa hivyo ni Dainess Koko Mwanafunzi kutoka shule ya sekondari Kalenga ameshukuru TASAF kwa kuwakumbuka wanafunzi wa kike kwani hapo mwanzo walikuwa wanashindwa kuhudhuria masomo kwa sababu ya changamoto ya ukosaji wa vifaa vya usafi.
"Mazingira ya shule yanakuwa hayarusu kwa binti aliye kwenye hedhi kwa sababu ya kukosa vifaa vya kufanyia usafi".
TASAF wametufanya tuone kuwa unapokuwa kwenye hedhi sio sababu ya kufanya kushindwa kuhudhuria masomo na kushindwa kufikia ndoto zako, Asante na Mungu awabariki msichoke kutuhudumia Alimalizia.
Ugawaji wa wa vifaa vya usafi umefanyika kama ulivyopangwa na vijiji ambavyo havikufanikiwa ni 52 ambapo vitapatiwa kipaumbele itakapojitokeza fursa nyingine.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa