UGONJWA WA TRAKOMA (VIKOPE) KUTOKOMEZWA IRINGA
Serikali kwa kushirikiana na shirika la Helen Keller International inaendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha ugonjwa wa Trakoma (vikope) unatokomezwa mkoani humo.
Akizungumza wakati wa zoezi la usawazishaji wa macho kwa wagonjwa katika kijiji cha Izazi Halmashauri ya Wilaya ya Iringa mapema leo 3 Machi 2023, Mratibu wa macho wa Mkoa Bi Jasmin Kachemela amesema zoezi hili linafanywa kwa hatua ambapo hatua ya kwanza ni ya mafunzo kwa wahudumu ngazi ya jamii (CHW), upimaji, matibabu kwa wagonjwa waliobainishwa na baadaye ufuatiliaji wa kina kwa wagonjwa waliopata matibabu kuhusu hali zao na kujiridhisha na uponaji wao.
Hivyo ametoa wito kwa watu wote wenye changamoto za macho zilizobainishwa na wahudumu kujitokeza ili kupata matibabu, “ vikope husababisha upofu na ni upofu wa kudumu kwa mtu kama hatapata matibabu kwa wakati” amesema.
Kwa upande wake Mratibu wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaombele wa Mkoa wa Iringa ndugu John Asukile Mwakabungu amesema lengo kuu la zoezi hili ni kuwa ugonjwa wa vikope (Trakoma) unatokomezwa kabisa hasa kwenye mkoa wa Iringa.
“tatizo sio kubwa sana kiasi cha kufanya tuanze kugawa dawa kwa kila mtu lakini lengo letu kuu ni kuhakikisha kuwa kupitia zoezi hili tunatokomeza kabisa ugonjwa huu, pia tunamshukuru mdau Helen Keller International kwa kujitokeza” amesema.
Vilevile wananchi waliofika kupata huduma ya usawazishaji wa macho (matibabu kwa njia ya upasuaji mdogo) kwenye zahanati ya Izazi wameishukuru serikali na mdau “Helen Keller International” kwa kuwafikishia huduma kijijini na kuongeza kuwa wao wasingeweza kuzifuata huduma hizi kwenye hospitali kubwa ikizingatiwa kuwa wengi ni wazee sana na hawana uwezo wa mumudu gharama za matibabu kwenye hospitali hizo.
Afisa mradi kutoka Helen Keller International Odiria Costantine amefafanua kuwa zoezi la kutoa mafunzo na utambuzi wa wagonjwa limefanyika kwa kata 13 za Halmashauri ya wilaya ya Iringa hadi sasa. Na matibabu kwa waliobainika na tatizo la vikope yanaendelea kutolewa ambapo hadi sasa tayari kata tisa (9) za Halmashauri ya Wilaya ya Iringa zimefikiwa na matibabu kutolewa. Idadi ya wagonjwa waliotibiwa hadi sasa ni 105 na zoezi linatarajiwa kufanyika kwa kata zote 28 za Halmashauri ya wilaya ya Iringa.
Pia Odiria Costantine, Afisa mradi ameshukuru kwa ushirikiano mkubwa uliotolewa na viongozi wa Mkoa pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa na kwamba hadi sasa zoezi la upimaji na utoaji wa matibabu kwa wagonjwa wa vikope linaendelea vizuri.
Kwa mjibu wa wataalamu wa afya inaelezwa kuwa Ugonjwa wa Trakoma (vikope) huambukizwa na bakteria ambao kichocheo kikubwa ni uchafu wa kwenye macho. Ili kuepuka au kujikinga na ugonjwa huu, watu hasa watoto wanashauriwa kunawa uso mara kwa mara kwa maji safi na sabuni.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa