Kikao Kazi cha Wakuu wa Shule na Walimu wa Kidato cha Tano na Sita
“Kwa kuweka nidhamu kati yenu Walimu na Wananfunzi, mnaweza kufuta daraja la nne na sifuri katika katika mitihani ya mwisho ya wanafunzi. Kwani nidhamu ni kitu cha kwanza kwa Mwalimu”.
Kauli hii imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Wakili Bashir Muhoja alipokuwa katika kikao kazi cha Wakuu wa Shule na Walimu wa Kidato cha Tano na Sita kilichofanyika leo tarehe 09/03/2023 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Siasa ni Kilimo.
Walimu hao wamekutana katika kikao kazi hicho ili kupeana mikakati ya kupandisha ufaulu kwa Kidato cha Sita, japo ufaulu upo vizuri. Hata hivyo pamoja na ufaulu huo, kuna baadhi ya Walimu wameshuka kiwango cha kufundisha kutokana na sababu mbalimbali.
“Napenda kuwahakikishia kuwa, madeni na stahiki mbalimbali mnazodai zitalipwa ikiwemo madeni ya likizo, uhamisho na malimbikizo mbalimbali”.
Akifafanua tatizo la ucheleweshaji wa madeni hayo Wakili Muhoja amesema kuwa, “Mtumishi anapokuwa na madai fulani ni lazima aombe kuandika barua akiainisha anachodai kwa wakati, na kwamba mtumishi anapochelewa kuomba stahiki zake ndipo ulipaji wa deni hili unapochelewa”.
Wakili Muhoja ameongeza kusema kuwa, japo mazingira wanayofanyia kazi Walimu ni magumu, amewaomba wasikate tamaa, pia wingi wa wanafunzi katika darasa moja ni moja kati ya jambo linalofifisha ufundishaji.
Aidha Wakili Muhoja amesisitiza suala zima la ushoga mashuleni kwa wanafunzi, jambo ambalo ni kilio kikubwa kwa Taifa. Ameomba Walimu kufuatilia na kuchunguza wanafunzi kama kuna viashiria vya vitendo hivyo ambavyo siyo maadili kwa tamaduni za Kiafrika.
Pia Wakili Muhoja amewaasa Walimu kutojihusisha na mahusinao ya kimapenzi na wanafunzi wa kike, kwani kufanya hivyo ni kinyume na kosa baada yake wajiheshimu na kuwaheshimu wanafunzi kwani ni wanafunzi hao ni kama watato wao.
Walimu nao wamepata nafasi ya kuzungumza kero na changamoto zao zikiwemo, uchache wa Walimu ikilinganishwa na idadi wa wanafunzi, miundombinu na motisha hata pale wanapofanya vizuri, kutolipwa madai yao kwa wakati na kutopandishwa madaraja.
Pamoja na changamoto hizo, Walimu hao wameahidi kujitoa kufundisha kwa moyo ikiwemo kufundisha muda wa ziada na siku za mwishoni mwa Juma ili kufikia malengo waliyojiwekea.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari Ndugu Sylivester Mwenekitete amewashukuru Walimu hao kwa kuitika wito na kueleza lengo la kikao hicho ni kuwekeana mikakati ya kupunguza au kuondoa Daraja Sifuri na Daraja la Nne.
Akizitaja shule zilizofanya vizuri kwa Mwaka wa Masomo wa 2022/2023 ni pamoja na Shule ya Sekondari Nyerere, Shule ya Sekondari Isimani, Shule ya Sekondari Kiwere, Shule ya Ufundi Ifunda, Shule ya Sekondari ya Wasichana Ifunda, Shule ya Sekondari Isimila, Shule ya Sekondari Tosamaganga, Shule ya Sekondari Idodi, Shule ya Sekondari Mtera na Shule ya Sekondari Pawaga.
Mwenekitete ameongeza kusema kuwa, “malengo yenu yatafikia vizuri ikiwa kutakuwa na ushirikiano ndani shule, baina ya shule na shule na ndani ya Halmashauri. Kwa kufanya hivi italeta mafanikio ya kiwango cha juu sana”.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu Bi. Beatrice Augustine alipokuwa anajibu hoja ya madai na stahiki mbalimbali za Watumishi amesema kwamba” kutokana na zoezi la kuhakiki vyeti, zoezi la upandishaji madaraja lilisitishwa lakini sasa hivi watumishi wanapandishwa vyeo na madaraja kama ilivyokuwa awali. Pia madai ambayo watumishi walikuwa wanadai wameanza kulipwa tangu mwaka wa fedha 2021/2022 hadi sasa yanaendelea kulipwa, na kwamba zaidi ya robo Tatu watumishi wamepanda madaraja.
Bi. Beatrice ameendelea kusema kuwa” hata watumishi ambao hawakupanda zaidi ya miaka kumi iliyopita, sasa hivi wameomba kibali kwa Katibu Mkuu ili waweze kupandishwa kwa utaratibu utakaolekezwa”.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa