WALIMU SHULE ZA SEKODARI IRINGA DC WANOLEWA KUHUSU MFUMO MPYA WA MALIPO KWA WAZABUNI NA WATOA HUDUMA
Walimu wa Shule za Sekodari katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa wapewa mafunzo ya kufanya malipo mbalimbali ya Shule kwa njia ya Mfumo mpya ambao wazabuni na watoa huduma wengine watafanyiwa malipo yao kwenye Mfumo wa Huduma ya TRA Kimtandao (Taxpayer Potal). Mafunzo haya yametolewa na wataalamu kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na Wahasibu kutoka Iringa Dc yaliyofanyika katika Ukumbi wa Siasa ni Kilimo tarehe 20.05.2023.
Kwenye mfumo huu, malipo ya mtoa huduma yatachakatwa na kodi ya zuio kukatwa kimtandao bila kumlazimu mtoa huduma kwenda kulipia kodi ya zuio mwenyewe jambo ambalo hapo kwanza lilileta usumbufu.
Akizungumza wakati wa mafunzo haya, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Wakili Bashir Muhoja amesema, lazima tujenge utamaduni wa kulipa kodi kwani makusanyo ya kodi baadaye hurudi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali akitolea mfano kuwa Shule zote za A-level katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa zinatarajia kupokea Fedha kutoka Serikalini muda wowote kutoka sasa kwa lengo la kuongeza madarasa na mabweni.
Kwa upande wake Meneja wa TRA Mkoa wa Iringa Ndg. Paul Walalaze amesema, Popote pale penye kipato kunatakiwa kuwa na kodi ya zuio na anayezuia ni mlipaji ambaye kwa hapa ni mtumishi wa Serikali. Aidha ndg. Walalaze amesema kodi ya zuio kwa mkandarasi ni 5% ya malipo yake na kwa mtoa huduma ni 2% ya malipo yake.
Pia amesisitiza kuhusu kudai risiti kwa kila manunuzi tunayofanya na kwamba kama ambavyo watumishi wa serikali wanalipa kodi bila kukwepa, vivyo hivyo na manunuzi mengine yote lazima kudai risi ili kujiridhisha na ulipwaji wa kodi.
Wakufunzi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Iringa na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa wametoa mafunzo hayo kwa minajili kuwa baada ya Mafunzo, kodi zote za zuio kutoka kwa wazabuni na watoa huduma wengine hazitalipwa na mzabuni au mtoa huduma bali zitalipwa Kimfumo na hivyo kodi ya serikali itazuiwa kabla ya fedha kumfikia mhusika.
Kundi lililopatiwa mafunzo ni mwalimu Mkuu wa Shule na mwalimu wa fedha wa Shule husika ambao kwa pamoja walipitishwa hatua kwa hatua juu ya namna ya kutumia mfumo hadi hatua ya mwisho ya kufanya malipo na kwamba kila mtoa huduma wa Shule au mzabuni lazima kwanza awe na TIN namba ndipo hatua zingine ziweze kuendelea.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa