WANAWAKE WAASWA KUTOKAA KIMYA WANAPOFANYIWA UKATILI ILI KUONDOA MAKOVU MIOYONI
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Veronica Kessy amewaasa wanawake kutokaa kimya pale wanapofanyiwa ukatili ili kuondoa makovu kwenye mioyo yao yanayotokana na kuumizwa.
Mh. Kessy ameyasema hayo alipokuwa akitoa Hotuba yake katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ambapo kwa Halmashauri ya Wilaya Iringa iliadhimishwa siku ya Tarehe 06/03/2023 kwenye Kata ya Migoli.
Aidha Mh. Kessy amesema kuwa Siku hii iliadhimishwa Kimataifa kwasababu wanawake walifanyishwa kazi ngumu, kunyimwa muda wa kunyonyesha na kulipwa ujira mdogo, Hivyo wakaanzisha siku hii 1975 ili kupinga mambo hayo na kupewa haki zao.
Kupitia Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu, Mh. Kessy amesema, Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wa Maendeleo wamekuwa wakishirikiana vema katika kuchochea maendeleo.
“Serikali yetu ikiongozwa na Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa mstari wa mbele kwa kushirikiana na Mashirika yasiyo ya Kiserikali kuchukua juhudi za makusudi za kuwaelimisha wananchi wote kuhusu masuala ya Ubunifu na Technolojia, kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu miongoni mwa wananchi. Juhudi nyingi za kuhakikisha wanawake wanakuwa wabunifu katika Nyanja za teknolojia ni pamoja na kuwapa nafasi ya kujiendeleza katika Nyanja za kielemu na kuwawezesha kiuchumi”
Aliendelea kusema kuwa, kwa kuwa mwanamke ni mlezi hivyo hapaswi kumwacha mtoto asiende shule. Njia pekee ya ukombozi ni Elimu. Pamoja na jitihada za Kiserikali za kuboresha miundombinu ya Elimu, lakini hadi sasa watoto 2149 hawajaripoti, 78% ndio wameripoti
Pia Mh. Kessy amewasisitiza wazazi na walezi kuhusu suala la malezi ya watoto ili kuwa na kizazi bora. Amesema tuangalie kwa makini katuni za watoto kwani kuna baadhi ya hizo katuni zinahamasisha ushoga.
Sanjari na hayo Mh Mkuu wa Wilaya amewashukuru wadau mbalimbali wa maendeleo na kutambua michango yao kwenye jamii. Miongoni mwa wadau hao ni World Vision Tanzania, Lyra in Africa, SOS Childrens, Philips, WWF & Care Alliance, na LTA.
Mh. Kessy amepokea na kukabidhi misaada mbalimbali iliyolenga kwenda kwa watoto na watu wenye uhitaji wa Kata ya Migoli kutoka kwa Waheshimiwa Madiwani, Shirika la World Vision Tanzania, Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, kikundi cha Ngoma Migoli na Viongozi wa Wanawake Chama cha Mapinduzi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mh. Stephen Mhapa ametoa pongezi kwa Diwani wa Kata ya Migoli Mh. Benitho Kayugwa, Diwani wa viti Maalumu Mh. Yuster Kinyaga, Mbunge wa jimbo la Isimani Mh. William Lukuvi na Watumishi wa Halmashauri wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji (W) kwa uhodari na uchapa kazi wao.
Pia Mh. Mhapa amewashukuru na kuwapongeza wadau wa maendeleo wanaoshirikiana na Serikali kufanya shughuli za maendeleo na kumwagiza Mkurugenzi Mtendaji (W) kuandaa taarifa ya Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali na Wadau wa maendeleo yanayofanya kazi kwenye maeneo ya Halmashauri na kumpatia Mh. Mkuu wa Wilaya ili aweze kuwatambua.
Aidha Diwani wa Migoli Mh. Benitho Kayugwa ametoa shukrani kwa shughuli nzima ya maadhimisho ya siku ya wanawake iliyofanyika Migoli Kiwilaya na kushukuru kwa misaada iliyotolewa na makundi mbalimbali kwenda kituo cha watoto yatima na watu wenye uhitaji, na kutumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kupitia Shirika la Akiba ya Chakula la Taifa (NFRA) kwa kutoa chakula kwa bei nafuu kwa wananchi wa Kata ya Migoli.
Mtaalamu wa Saikolojia na Afya ya Akili Ndugu Baraka Mshobozi ametoa elimu ya saikolojia ili kukabiliana na madhara yatokanayo na ukatili wa kijinsia. Pia mtaalamu kutoka Dawati la jinsia la Jeshi la Polisi alitoa elimu juu ya ukatili wa kijisia na hatua mbalimbali zinazopaswa kuchukuliwa ili kuzuia ukatili.
Maadhimisho ya siku ya wanawake duniani mwaka 2023 yamebebwa na Kauli Mbiu isemayo,”Ubunifu na Mabadiliko ya Teknolojia, Chachu Katika Kuleta ustawi wa Kijinsia”
@tamisemi
@samiasuluhuhassan
@angelakairuki
@msemajimkuuwaserikali
@halimadendego
@veronicakessy
@iringars
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa