“Watendaji Wanaovujisha na Kuiba Mapato, Hawatafumbiwa Macho” – Mh. Mhapa
“Watendaji wanaovujisha na kuiba mapato ya Serikali hawatafumbiwa macho hata kidogo. Kama wewe una dhamana ya kukusanya mapato kisha unaachia mapato yanapotea na kuibiwa utachukuliwa hatua kali za kisheria”.
Kauli hii imetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Stephen Mhapa alipokuwa anatoa hotuba yake katika siku ya Pili ya Mkutano wa Baraza la Madiwani uliofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri Ihemi Februari 27, 2024.
Aidha, Mheshimiwa Mhapa amendeelea kusema kuwa, jambo la kukusanya mapato si la Mkurugenzi peke yake, jambo hili ni la kila mtu na anatakiwa kuwajibika, na hasa sehemu zote zilizowekwa mashine ya kukusanyia mapato (PoS)”.
Mkutano huo ulianza Februari 26, 2024 kwa kutoa taarifa za Kata, pia Mheshimiwa Mhapa ambaye alikuwa akiongoza Mkutano huo alisema machache, “Kutokana na maafa makubwa ya mvua zinazoendelea kunyesha bahati mbaya tulipoteza mtu mmoja hadi sasa. Naendelea kusisitiza wananchi wachukue tahadhari kwani bado mvua zinaendelea kunyesha”.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Veronica Kessy amesema, usalama wa Wilaya upo vizuri, kadhalika hali ya siasa.
Mheshimiwa Kessy, amemshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuleta fedha nyingi za miradi hivyo tuwajibike kwa kila mtu sehemu yake kukamilisha miradi hiyo ili fedha zisirudi.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya Komredi Rehema Mohamedi amesema, kutokana na vijiji vingi kukosa Watendaji, amemuomba Mwenyekiti wa Halmashauri kufuatilia kwa Waziri wa Utumishi ili kutoa kibali cha kuajiri Watendaji hao, ifikapo uchaguzi Watendaji hao wawe wameshazoea mazingira ya kazi.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya Komredi Costantine Kihwele amempongeza Mkurugenzi Mtendaji Wakili Bashir Muhoja kwa mapokezi ya fedha hizo na kuzipangia katika miradi ya maendeleo kama inavyohitajika hasa sehemu ambazo zina upungufu mkubwa wa madarasa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Wakili Bashir Muhoja amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo hasa elimu. Wakili Muhoja ameahidi kuanza kutekeleza miradi hiyo mara moja kwani fedha zimeshasoma na kupangiwa vifungu.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa