WATENDAJI KATA WILAYANI IRINGA WAAGIZWA KUSIMAMIA UTOLEWAJI WA CHAKULA SHULENI.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Veronica Kessy amewataka Watendaji wa Kata zote zilizopo wilayani humo kusimamia utolewaji wa vyakula kwenye shule zote ikiwa ni moja ya mpango mkakati wa kutokomeza udumavu.
Mh. Kessy alisema hayo alipokuwa kwenye kikao cha kawaida cha Tathmini ya Mkataba wa Lishe kilichofanyika tarehe 21.03.2023 katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo.
Alisema “Mkataba wa Lishe unawawajibisha Watendaji wote kusimamia masuala yote ya Lishe ikiwemo kuhakikisha kuwa kila shule inatoa chakula cha mchana kwa wanafunzi”
Aidha, Mh. Kessy amewapongeza Watendaji wa Kata zilizoweza kutoa chakula kwa wanafunzi kwenye shule zote na kuwataka wengine waliobaki kufanya hivyo katika shule zilizopo katika Kata zao.
Hata hivyo, Mheshimiwa Kessy ameshangazwa na hali ya udumavu iliyopo Mkoani Iringa hususani katika Wilaya hiyo licha ya Mkoa wa Iringa kubarikiwa na uwepo wa vyakula vingi, hivyo kumtaka Afisa Lishe asaidie namna bora ya ulaji utakaosaidia kuondokana na hali hiyo.
Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Dkt. Samweli Marwa ametahadharisha juu ya takwimu zinazotumika kutathmini hali ya Lishe ndani ya mkoa huo, kwani zinaleta hali isiyo na ulinganifu na uhalisia.
Kwa upande wake Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Bi. Tiliza Mbulla amesema kuwa pamoja na changamoto mbalimbali za masuala ya lishe pia kuna mafanikio yaliyofikiwa, ikiwa ni pamoja na ongezeko la wanafunzi wanaopata angalau mlo mmoja shuleni kutoka 69.84% hadi 78.69% kwa kipindi cha Oktoba-Desemba 2022, ongezeko la idadi ya shule zinazotekeleza mpango wa Lishe kutoka 70.73% hadi 87.44% kwa kipindi cha Okt-Dec 2022 na utekelezaji wa viashiria vyote vya mkataba wa Lishe kwa ufanisi kwa kutumia fedha za Halmashauri.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa