Watendaji Wahimizwa Kuwatembelea Wajawazito na Wazazi Wanaonyonyesha
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Veronica Kessy, amewataka Watendaji wa Kata kwa kushirikiana na Watoa Huduma za Afya kuwatembelea akina Mama Wajawazito na Wazazi wanaonyonyesha kuwapa elimu ya umuhimu wa lishe bora ili kuepukana na udumavu.
“Kuna baadhi ya Kata hazijatembelewa na Watoa huduma za afya, kuongea na wazazi wanaonyonyesha na wajawazito kuwapa elimu ya umuhimu wa lishe bora yenye milo mitatu kwa siku. Hii inasababisha kuleta asilimia chini ya 100 kwa kutotekeleza. Hivyo nawasisitiza kufanya hivyo ili kipindi cha Robo ya Tatu kuwepo na utekelezaji wa 100% kwa kila Kata. Kufanya hivyo kutaleta matokeo chanya kwenye suala zima la udumavu”.
Mheshimiwa Kessy ameyasema hayo alipokuwa anatoa hotuba katika kikao cha Tathimini ya Mkataba wa Lishe kwa Robo ya Pili (Oktoba – Desemba) kwa mwaka wa Fedha 2023/2024.
Mheshimiwa Kessy ameendelea kusisitiza kuwa, Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo ya Surua imeanza, na kuwataka Watendaji kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupeleka watoto kupata chanjo hiyo. Watoto wanaotakiwa kupata chanjo ni wenye umri wa miezi 0 – 9.
Aidha Mheshimiwa Kessy amewataka Watendaji hao kusimamia usafi wa mazingira ya maeneo yao, kutatua kero mbalimbali za wananchi, kwani mwaka huu ni uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kusiwepo sababu za wagombea kukosa kura.
Isitoshe Mheshimiwa Kessy amewataka Watendaji kutojihusisha na masuala ya kisiasa, na kuwataka kusimamia haki kwa kila jambo linalojitokeza.
Akiwasilisha taarifa ya Muongozo wa Chakula na Ulaji Tanzania Bara Afisa Lishe wa Halmashauri Bi. Tiliza Mbulla amesema, Muongozo huo ulitolewa mwaka 2023 na kusambazwa Januari 2024.
Lengo la Muongozo huo ni kuboresha hali ya Lishe na Afya za watu wa rika na makundi yote katika jamii ya Watanzania.
Bi. Tiliza amesema, Mwongozo wa Kwanza ni kula vyakula mchanganyiko kutoka makundi sita ya chakula kila siku. Mwongozo wa Pili ni kujitahidi kufikia lishe inayopendekezwa na akina mama wajawazito na wanaonyonyesha watoto wachanga ili kuhakikisha afya bora ya mama na ukuaji wa mtoto. Muongozo wa Tatu ni kupunguza ulaji wa vyakula vilivyokaangwa na mafuta mengi. Mwongozo wa Nne ni kuhakikisha ussafi wa mazingira mahali unapoishi. Muongozo wa Tano ni kuwa na mtindo bora wa maisha ili kupata afya bora n uzito unaoshauriwa na Muongozo wa Sita ni kuepuka tabia hatarishi kama vile matumizi ya sigara na unywaji wa pombe ili kupunguza hatari ya kupata magonjwa.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa