Mkuu Wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu Iringa DC Bi. Beatrice Augustino amesema kuwa changamoto mbalimbali zinazohusiana na masuala ya utumishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa zikiwemo za wauguzi zimefanyiwa kazi na kama zipo zilizosalia zifikishwe kwenye ofisi husika ili nazo ziweze kushughulikiwa.
Bi. Beatrice ameyasema hayo alipokuwa akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani ambapo Kiwilaya yamefanyika katika kijiji cha Nzihi Mei 18, 2024.
Aidha, Bi. Beatrice amempongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya mambo makubwa katika uongozi wake ikiwemo kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi hadi 23%, kulipa madai ya watumishi pamoja na malimbikizo ya mshahara ambapo zaidi ya Bilioni 2.1 zimelipwa kama malimbikizo ya mshahara kwa watumishi wa Iringa DC na madai mengine Zaidi ya 210 yamewasilishwa Ofisi ya Rais Utumishi ili kufanyiwa kazi, Watumishi Zaidi ya 2005 kati ya watumishi 3347 wamepandishwa madaraja na wengine kubadilishiwa miundo ya kiutumishi.
Pamoja na mambo yaliyoelezwa pia wataalamu wa afya kada Uuguzi wamekumbushwa haki na wajibu na kwamba hivi ni vitu viwili vinavyoendana. “Tunapodai Haki, tuhakikishe tumetimiza wajibu wetu ipasavyo” amesema Bi. Beatrice.
Naye Mkuu wa Idara ya Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Dkt. Samweli Marwa amewapongeza wauguzi kwa kazi nzuri na kuwaahidi kuwa wataendelea kuzitatua changamoto mbalimbali za kazi na vitendea kazi kwa kadri watakavyokuwa wanapata rasilimali na yale yaliyo nje ya uwezo wa halmashauri wataendelea kuyawasilisha Wizarani ili kupata utatuzi.
Maadhimisho haya yamefanyika kwa kuambatana na kufanya matendo ya huruma ambapo wauguzi walitembelea Kituo cha kulelea watoto yatima cha Nzihi kutoa msaada wa vyakula. Vile vile kwa tawi la Tosamaganga wametoa huduma za vipimo vya saratani ya mlango wa kizazi, magonjwa yasiyoambukiza, upimaji wa VVU bure na huduma ya RCH.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa