Waziri Jafo Aagiza Waliovamia Vyanzo vya Maji Kuondoka Mara Moja
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa maagizo kwa wananchi wote waliovamia vyannzo vya maji kuondoka haraka iwezekanavyo na pia ameiagiza Mamlaka za Mabonde kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaochepusha maji kinyume cha sheria.
Waziri Jafo ameziagiza Mamlaka za Mabonde kote nchini kuhakikisha wanasimamia sheria ya maji kwa kuangalia pia wale wote waliopata vibali vya kutumia maji hayo kuhakiki kama maji hayo yanatumika kwa kuzingatia sheria na utaratibu lengo kubwa likiwa ni kuendelea kutunza maji katika maeneo yetu.
Ameyasema hayo leo tarehe 15 Novemba, alipokua katika ziara ya kutembelea na kukagua madhara ya kimazingira yaliyotokana na changamoto za ukame katika Mto Ruaha unaopatikana katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha na kisha kufanya mkutano kujadili changamoto hizo na kuona ni kwa namna gani changamoto hizo zinaweza kutatuliwa.
"...Hali hii imesababisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa maelekezo kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kufanya kazi ya kufanya tathmini kwa kina hali inayoendelea na nini kifanyike ile tuiokoe nchi yetu, na ndio maana leo tupo hapa ". Amesema.
Aidha ameipongeza Serikali ya Mkoa wa Iringa na Mbeya kwa kuendesha kampeni ya kuondoa mifugo katike sehemu ya chanzo cha maji Ihefu ambayo iko mkoani Mbeya na pia ameishukuru TANAPA kwa kuendelea kuitunza hifadhi.
Waziri Jafo amesema shughuli za kibinadamu ndio chanzo kikuu cha kukauka kwa Mto Ruaha mkuu wakiwemo wakulima ambao wamekuwa wakichepusha maji bila kujali utaratibu wa maji, na ukataji wa miti uliokithiri, na kupelekea ukame ulioonekana kwa dhahiri.
Amesema timu ya wataalamu itapeleka mapendekezo kwa Viongozi wa juu kuhusu nini kifanyike kadhalika amesema kamati hiyo ya viongozi waliohudhuria wamekubaliana kuwa wale wote waliovamia vyanzo vya maji kuondoka mara moja kuanzia leo hii, pia shughuli zote zinazoendelea lazima zizingatie sheria zote zikiwemo zile za mazingira.
Mkutano huo umewakutanisha Mawaziri mbalimbali wakiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Seleman Jafo, Waziri wa Utalii na Maliasili Mhe. Dkt. Pindi Chana, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo na Makazi Mhe. Dkt. Angelina Mabula, Waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Anthony Mavunde, Katibu Mkuu Wizara ya TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe na Wakuu wa Mikoa nane wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Halima Dendego, Wakuu wa Mikoa wengine ni pamoja na Mbeya, Dodoma, Njombe, Kigoma, Tabora, Morogoro, Pwani, Katavi, Rukwa, Songwe.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa