Afisa TEHAMA Iringa DC: Tujiepushe na Matapeli wa Mtandao
Afisa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Halmashauri ta Wilaya ya Iringa Ndugu Christopher Aron Mfugale amewataka Watumishi wa Halmashauri kuacha kutoa Nywira za akaunti za mifumo mbalimbali ya serikali amesema kufanya hivyo kunaweza kupelekea kuvuja kwa taarifa za serikali.
Changamoto zote zinazohusu masuala ya mfumo yanatatuliwa na Wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Iringa na si vinginevyo, amesisitiza kuwa mtumishi anapopata changamoto asikimbilie katika vibanda vya intaneti na badala yake awasiliane na ofisi ya TEHAMA Wilaya kwa wakati wowote ule.
Ameyasema hayo alipokuwa akiwasilisha mada ya Matumizi sahihi ya TEHAMA kwa Watumishi ikiwa ni siku ya pili ya Maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika 25.06.2022, katika Kata ya Idodi, Shule ya Sekondari Idodi ambapo Watumishi mbalimbali kutoka maeneo tofauti tofauti Kata ya Idodi pamoja na wataalamu kutoka Makao Makuu wamekutana kuadhimisha wiki hiyo.
Amesema kuwa Watumishi wa Umma wana nafasi kubwa kwa jamii katika kuwaelimisha juu ya matumizi sahihi ya risiti, kudai na kutoa risiti pale unaponunua na kuuza kitu, bidhaa, huduma au rasilimali yoyote ile.
"Tunatakiwa tuwe wajumbe wazuri wa kufikisha hii elimu kwa wananchi hata kwa wakusanyaji wa mapato kutoka Halmashauri yetu, Kwani mapato yakiongezeka ndivyo maendeleo yatakavokuja katika Halmashauri yetu".
Amesema pia Serikali kwa sasa imekuja na mfumo mzuri na bora wa kupokea maoni, ushauri, kero, changamoto pamoja na pongezi kutoka kwa Watumishi na wananchi kuelekea kwa Taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.
Akifafanua amesema kuwa mfumo huu utarahisisha kuokoa gharama za nauli pamoja na muda ambapo hapo awali ilikuwa mpaka utoke katika kituo chako cha kazi na kwenda Makao Makuu ya Taasisi kwa ajili ya kuwasilisha tatizo au hoja yako kuhusu jambo fulani lakini kwa sasa huduma hii itapatikana kwa njia ya mfumo rasmi.
"Kuna njia mbili za kuingia katika mfumo huu, Njia ya kwanza ni kwa intanenti ambapo Mtumishi anatakiwa kuwa na simu janja pamoja na bando la intanenti ambapo ataingia katika kivinjari chake na kuandika emrejesho.gov.go.tz kisha atafuata maelekezo. Njia ya pili ni njia ya kawaida ambapo Mtumishi au Mwananchi atatakiwa kupiga *152*00# kisha kuchagua namba 9 kisha kuendelea. Huduma hii ni bure na inapatikana mitandao yote".
Aidha amewasisitiza watumishi wote kupenda kutembelea na kuhamasisha wananchi kufuatilia Tovuti ya Halmashauri ya Wilaya ili kujua taarifa zote zinazohusu Halmashauri zikiwemo shughuli za miradi inayopangwa kutekelezwa, iliyokamilika na inayoendelea. Pia taarifa na matukio mbalimbali ya Serikali huwa yanachapishwa huko.
"Nia ajabu kuona kuwa Mtumishi wa Halmashauru yetu hajui kuwa tuna tovuti ya Halmashauri wala mitandao ya kijamii, Ninawaomba muwe mnafatilia tovuti yetu ni www.iringadc.go.tz na pia Facebook ni Iringa Dc, Instagram ni Iringa_Dc mfuatilie na muwaambie na wenzenu ambao hawapo hapa".
Maadhimisho haya ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanatarajiwa kuendelea siku ya Jumatatu 27.06.2022 katika Tarafa ya Pawaga.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa