Baraza la Madiwani Lapitisha Hesabu za Mwaka wa Fedha 2021/2022
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Steven Mhapa leo Septemba 29, 2022 ameongoza Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani wa kupitia taarifa ya hesabu za Mwaka wa Fedha unaoishia Juni 30, 2022 uliofanyika katika Ukumbi wa Siasa ni Kilimo.
Akiwakilisha taarifa hiyo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Bi. Beatrice Augustine amesema, “kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya mwaka 1982 pamoja na marekebisho yake na mwongozo wa fedha wa Serikali za Mitaa, Halmashauri ina wajibu wa kuandaa taarifa ya hesabu za mwisho wa mwaka wa fedha na kuziwasilisha kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kabla au ifikapo Septemba 30 ya kila mwaka”.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Iringa Ndugu Estomin Kyando akichangia hoja katika mkutano huo amesema, “kwa kushirikiana na DT, Mkaguzi wa Ndani na Nje mnatakiwa kupitia tena taarifa hii ili kujiridhisha na hatimaye kusiwe na maswali kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mhe. Mathew Markus Nganyagwa amewaagiza Wataalamu wa Halmashauri kufanyia marekebisho sehemu zote ambazo wameelekezwa na Wajumbe ili kuondoa kujirudia kwa makosa ambayo tayari yameshatolewa ufafanuzi, amesisistiza pia suala la kufanya kazi kwa makini.
Wajumbe wa Mkutano huo wamepitisha taarifa hiyo kwa kauli moja, na kuahidi kufanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa na Wajumbe huku wakiamini kwamba, Halmashauri ya wilaya ya Iringa itaendelea kupata hati safi kutokana na hesabu kuandaliwa kwa kuzingatia matakwa yote ya sheria na miongozo mbalimbali ya ufungaji wa Hesabu za Serikali.
Kijiji cha Ihemi
Anuani ya posta: Po.Box108 Iringa
Simu ya mezani: 026-2702828/2702585
Simu ya mkononi: 0757 364 994
Barua pepe: ded@iringadc.go.tz
Haki miliki @ Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Haki zote zimehifadhiwa